Mbunge wa Jimbo la Kibamba ambaye pia ni Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, amekabidhiwa tuzo ya kutambua mchango wake katika maendeleo ya sekta ya elimu katika Manispaa ya Ubungo.
Tuzo hiyo imetolewa Julai 31, 2026, katika hafla ya utoaji wa tuzo kwa wanafunzi, walimu, shule na wadau waliofanya vizuri katika matokeo ya Mitihani ya Kumaliza Elimu ya Msingi na Upimaji wa Kitaifa kwa mwaka wa masomo 2025, iliyofanyika katika Ukumbi wa Anazak, Temboni. Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mhe. Kairuki ameishukuru Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa kutambua mchango wa wadau wa elimu, akisema hatua hiyo ni motisha kwa wadau kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuinua kiwango cha elimu.
Amesema elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa, hivyo Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka mazingira bora yatakayowezesha watoto kupata elimu yenye ubora.
Pia amewapongeza wanafunzi, walimu, wazazi na wadau wote waliochangia mafanikio makubwa ya matokeo ya elimu ya msingi katika Manispaa ya Ubungo ikiwemo katika Jimbo la Kibamba.
Hafla hiyo ilitumika kutambua na kutoa tuzo kwa wanafunzi, walimu, shule na wadau mbalimbali waliotoa mchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya elimu, kufuatia kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu katika mitihani ya Darasa la Nne na Darasa la Saba kwa mwaka wa masomo 2025.
