Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amemtaka Balozi mteule wa Tanzania nchini Malaysia, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy, kutumia nafasi hiyo kuimarisha zaidi uhusiano wa Tanzania na Malaysia pamoja na kuongeza fursa za uwekezaji.
Dkt. Nchimbi ametoa kauli hiyo leo Agosti 20, 2026, mkoani Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi Mkeremy.
Makamu wa Rais amempongeza Balozi Mkeremy kwa uteuzi huo uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa Malaysia ni nchi yenye uchumi mkubwa na ambayo ina ushirikiano wa kimkakati na Tanzania katika maeneo mbalimbali, ikiwemo biashara na majukwaa ya kimataifa.
Amemtaka Balozi Mkeremy kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kuongeza fursa za ushirikiano, kuvutia wawekezaji zaidi kutoka Malaysia na kuhamasisha Watanzania wanaoishi nchini humo kuwekeza Tanzania.
Aidha, Dkt. Nchimbi amemtaka Balozi huyo kufahamu kwa kina Dira ya Taifa 2050 pamoja na Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030 ili kuzingatia vipaumbele vya Taifa katika utekelezaji wa majukumu yake ya kidiplomasia.
Kwa upande wake, Balozi mteule Mkeremy amemshukuru Rais Samia kwa kumwamini na kumteua kuiwakilisha Tanzania nchini Malaysia.
Pia amemshukuru Makamu wa Rais kwa ushauri na maelekezo aliyompa, akiahidi kuyatekeleza kwa ufanisi katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Malaysia.
