AWESO AELEKEZA KITUO CHA AFYA MASIEDA M-MBULU KUKAMILIKA KWA WAKATI


Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Hamidu Aweso (Mb), amekagua ujenzi wa Kituo cha Afya Masieda kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, mkoani Manyara, na kusisitiza kuwa awamu ya pili ya mradi huo ikamilike kwa wakati ili wananchi waanze kunufaika na huduma bora za afya. Kituo hicho kinatarajiwa kuhudumia wakazi 7,865 wa Kata ya Masieda na maeneo ya jirani, ambao kwa muda mrefu walikuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya.

Mradi huo wenye thamani ya Shilingi milioni mia tano themanini na sita, elfu thelathini na mbili na mia moja arobaini na mbili (Sh. 586,032,142.00), unaotekelezwa kwa fedha za Serikali Kuu, unahusisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la maabara, jengo la mama na mtoto, jengo la upasuaji, jengo la kufulia pamoja na kichomea taka. Hadi sasa, Shilingi milioni mia tano arobaini na sita, elfu thelathini na mbili (Sh. 546,032,000.00) zimetumika katika utekelezaji wa mradi huo, huku Shilingi milioni arobaini, mia moja arobaini na mbili (Sh. 40,000,142.00) zikitengwa kukamilisha kazi zilizobaki.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Mhe. Aweso amesema awamu ya pili ya utekelezaji itahusisha ununuzi wa vifaa tiba na vifaa vingine muhimu ili kituo hicho kianze kutoa huduma kwa wakati. Aidha, ameeleza kuwa changamoto ya upatikanaji wa nguzo za umeme itatatuliwa ili kuwezesha kufikishwa kwa umeme na huduma ya maji katika kituo hicho, akisisitiza kuwa Serikali haitaruhusu changamoto hizo kuchelewesha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Aweso pia amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwekeza katika kuboresha huduma za kijamii kupitia sekta za afya, maji na elimu. Amesema pamoja na ujenzi wa vituo vya afya na miradi ya maji, Serikali inaendelea kujenga shule na kuimarisha miundombinu mingine ya maendeleo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na maendeleo yanafika katika kila kona ya nchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post