WAZIRI HOMERA AIPONGEZA KOREA KWA KUANDAA KIKAO CHA 48 CHA KAMATI YA URITHI WA DUNIA YA UNESCO


Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Dkt. Juma Zuberi Homera (Mb.), ameipongeza Jamhuri ya Korea kwa kufanikiwa kuwa mwenyeji wa Kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO (48th Session of the World Heritage Committee), kinachofanyika katika Jiji la Busan kuanzia tarehe 19 hadi 29 Julai 2026.

Akichangia katika mjadala wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Homera aliishukuru UNESCO kupitia Kituo cha Urithi wa Dunia (World Heritage Centre) kwa kuendelea kutoa usaidizi wa kitaalamu kwa nchi za Afrika, ikiwemo Tanzania, licha ya changamoto za kifedha zinazoikabili taasisi hiyo.

Aidha, alisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana kikamilifu na UNESCO katika kipindi chake cha uanachama wa Kamati ya Urithi wa Dunia ili kuhakikisha malengo na misingi ya Mkataba wa Urithi wa Dunia wa mwaka 1972 yanaendelezwa na kutekelezwa kwa ufanisi.

Katika mjadala kuhusu ushirikishwaji wa Watu wa Asili katika utekelezaji wa Mkataba wa Urithi wa Dunia wa mwaka 1972, Mheshimiwa Homera alieleza kuwa Tanzania inatambua kuwepo kwa Azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 2007 kuhusu Haki za Watu wa Asili (United Nations Declaration on the Rights of Indigenous Peoples – UNDRIP). Hata hivyo, alibainisha kuwa azimio hilo halina nguvu ya kisheria inayowafunga wanachama wa Umoja wa Mataifa. Vilevile, alieleza kuwa Mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO Convention No. 169), ambao unahusu Watu wa Asili na wa Kabila, umeridhiwa na idadi ndogo ya nchi duniani.

Kutokana na hali hiyo, Tanzania iliomba ufafanuzi kuhusu msingi wa kisheria na namna ambavyo UNESCO inapendekeza kujumuisha ushirikishwaji wa Watu wa Asili katika utekelezaji wa Mkataba wa Urithi wa Dunia wa mwaka 1972, hususan pale ambapo hakuna wajibu wa kisheria unaotokana na vyombo husika vya kimataifa.

Kikao hicho kinaendelea hadi tarehe 29 Julai 2026. Katika kipindi cha mkutano huo, tarehe 27 Julai 2026, Tanzania inatarajiwa kuandaa mkutano wa pembeni (Side Event) utakaotoa fursa ya kuzungumzia masuala mbalimbali yanayohusu uhifadhi, usimamizi na maendeleo endelevu ya Urithi wa Dunia.

Post a Comment

Previous Post Next Post