USALAMA NI NGUZO YA MAENDELEO YA UCHUMI - DKT. NYASAHO


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka wahitimu wa Kozi ya Usalama na Stratejia ya Chuo cha Ulinzi wa Taifa (NDC) kutumia maarifa na ujuzi walioupata kuimarisha usalama wa taifa pamoja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Samia katika mahafali ya wahitimu hao, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb), amesema kuwa maendeleo ya uchumi wa taifa yanategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa wataalamu wenye uelewa wa masuala ya usalama na stratejia, ambao huchangia kulinda amani na mazingira wezeshi ya maendeleo.

Dkt. Nyansaho amewasisitiza wahitimu hao kutumia taaluma waliyoipata kwa weledi, uzalendo na uwajibikaji ili kuendelea kuimarisha taasisi zao na kushiriki kikamilifu katika kukabiliana na changamoto za kiusalama zinazoibuka ndani na nje ya mipaka ya nchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Ulinzi wa Taifa, Balozi Meja Jenerali Wilbert Ibuge, amemhakikishia Waziri wa Ulinzi kuwa wahitimu wote wamepata mafunzo yenye viwango vinavyotambulika kimataifa, yanayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika sekta ya ulinzi na usalama.

Jumla ya wahitimu 72 kutoka mataifa 17 walihitimu kozi hiyo. Mataifa hayo ni Bangladesh, Burundi, Botswana, Rwanda, Uganda, Kenya, Malawi, Zambia, Zimbabwe, Nigeria, India, Ethiopia, Namibia, Afrika Kusini, Sierra Leone, Misri na Tanzania, jambo linaloendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya ulinzi na usalama.

Post a Comment

Previous Post Next Post