Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kuhakikisha mpango wa kuifufua Reli ya TAZARA unatekelezwa kwa ufanisi ili kurejesha hadhi yake kama mhimili muhimu wa biashara, usafirishaji na maendeleo ya uchumi wa Tanzania, Zambia na ukanda wa Kusini mwa Afrika.
Amesema hayo leo Julai 14, 2026, katika hafla ya chakula cha jioni ya maadhimisho ya miaka 50 ya TAZARA iliyofanyika Serena Hotel jijini Dar es Salaam.
Profesa Mbarawa amesema TAZARA ni urithi wa ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania, Zambia na China uliojengwa chini ya uongozi wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Dkt. Kenneth Kaunda na Mwenyekiti Mao Zedong, ikiwa ni reli iliyosaidia ukombozi wa Kusini mwa Afrika na kuimarisha uhuru wa kiuchumi wa Zambia.
Ameongeza kwa kusema kuwa, licha ya mchango wake mkubwa, TAZARA imekabiliwa na changamoto za miundombinu chakavu, upungufu wa mabehewa na injini pamoja na kushuka kwa mizigo na mapato, hali iliyozifanya Serikali za Tanzania na Zambia kutafuta suluhisho la kudumu la kuifufua reli hiyo.
Waziri Mbarawa amebainisha kuwa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Rais Hakainde Hichilema wa Zambia wameonesha uongozi madhubuti kwa kusimamia mpango wa kuhuisha TAZARA kwa kushirikiana na Serikali ya China, ili kuboresha reli, kuongeza vifaa vya kisasa, kuimarisha huduma na kujenga taasisi endelevu yenye ushindani.
Amesema uboreshaji wa TAZARA utaongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, kupunguza gharama za usafirishaji, kuimarisha biashara ya madini, mazao na bidhaa mbalimbali, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kikanda.
Aidha, amewataka menejimenti, wafanyakazi, wawekezaji na wadau wote kutekeleza majukumu yao kwa uwajibikaji ili kuhakikisha reli hiyo inakuwa chachu ya maendeleo kwa vizazi vijavyo.
