Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo Tanzania (TIB), Bw. Deogratius Kwiyukwa, amesema kuwa uunganishaji nguvu ya pamoja ya Taasisi za kifedha katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC, utachochea ujenzi wa viwanda vitakavyokuwa chachu ya kukuza maendeleo ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo kiuchumi na kijamii.
Bw.
Kwiyukwa, amesema hayo kando ya Mkutano wa 9 wa Wiki ya Viwanda ya SADC (SADC
Industrialisation Week) unaoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa
(ICC), jijini Durban, nchini Afrika Kusini.
Alisema kuwa TIB ambayo ni Taasisi ya Serikali imeshiriki katika mkutano huo
kutafuta fursa za kushirikiana na taasisi nyingine za kifedha ndani ya ukanda
wa SADC ili kuunganisha mitaji kwa ajili ya kufadhili miradi mikubwa ya
maendeleo itakayo changia kufikia lengo la utekelezaji wa DIRA ya Taifa ya
Maendeleo 2050 inayotaka uchumi wa Tanzania ufikie thamani ya dola za Marekani
trilioni moja ifikapo mwaka huo.
Bw. Kwiyukwa alisisitiza kuwa ujenzi wa viwanda vitakavyoongeza thamani ya
bidhaa za kilimo, madini adimu, na bidhaa nyingine vitakavyochochea ajira na
mauzo ya nje unahitaji uwekezaji mkubwa wa mitaji.
Alisema
kuwa Tanzania imewekeza kwenye reli ya SGR, bandari, nishati, barabara na
usafirishaji, hatua inayofuata ni kuhakikisha mali hizo zinazalisha shughuli za
kiviwanda kuunganisha SGR, bandari, umeme na hifadhi za viwanda, kanda maalum
za kiuchumi, maeneo ya madini, vituo vya kilimo na masoko ya nje.
Alisema
kuwa TIB, kwa kushirikiana na Taasisi nyingine za Fedha za Ukanda wa SADC,
inaweza kufadhili mifumo mizima ya kiuchumi inayozunguka miundombinu hiyo ya
reli inayochochea viwanda kando ya njia yake, bandari inayosaidia biashara ya
ghala na usafirishaji, umeme wa uhakika unaovutia viwanda vinavyotumia nishati
nyingi.
Alisema
kuwa mpaka sasa TIB imeviwezesha viwanda na sekta nyingine kadhaa za umma
kupata mikopo nafuu kwa ajili kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kama vile
kahawa, sukari, miradi ya maji na kwamba ikiwezeshwa zaidi kimtaji itafanya
mambo makubwa zaidi.
Baadhi ya
Washiriki wa Mkutano huo wamebainishwa kuwa wamevutiwa na fursa nyingi
zinazopatikana nchini Tanzania na kuahidi kutafuta taarifa zaidi za maeneo
wanayotaka kuwekeza.
Mkutano wa
9 wa Wiki ya Viwanda wa SADC umewakutanisha viongozi wa serikali, sekta
binafsi, wawekezaji, taasisi za kifedha, wataalamu na wadau wa maendeleo kutoka
nchi wanachama wa SADC na unafanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Kukuza
Viwanda Imara, Endelevu na Jumuishi kupitia Maendeleo ya Miundombinu, Mageuzi
ya Kilimo na Madini kwa Ajili ya Dunia Yenye Haki.”
Kwa ujumla, mijadala ya Mkutano wa Wiki ya Viwanda wa SADC jijini Durban
imeweka msisitizo mkubwa katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kuongeza
thamani ya rasilimali za madini na bidhaa nyingine kabla ya kuuzwa nje, pamoja
na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda, miundombinu na miradi ya
maendeleo.
