TARURA YAFUNGUA FURSA ZA AJIRA KUPITIA MATENGENEZO YA BARABARA, VIKUNDI 1,400 KUNUFAIKA 2026/27


Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeendelea kupanua Mpango wa Matengenezo ya Kawaida ya Barabara kwa Ushirikishwaji wa Jamii (Community-Based Routine Maintenance – CBRM), unaolenga kuboresha miundombinu ya barabara sambamba na kutoa fursa za ajira na kipato kwa wananchi.

Mpango huo unaotekelezwa chini ya Mradi wa RISE unaofadhiliwa na Serikali kupitia mkopo kutoka Benki ya Dunia, unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu ya fedha kuanzia mwaka 2025/26 hadi 2027/28.

Mratibu wa Mpango wa CBRM kutoka TARURA Makao Makuu, Mhandisi Richard Missa, amesema mpango huo unalenga kuboresha zaidi ya kilomita 15,000 za barabara nchini huku ukiwezesha zaidi ya vikundi 3,000 vya wananchi kushiriki katika shughuli za matengenezo ya barabara.

Amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, utekelezaji wa mpango huo umeanza kwa mafanikio ambapo vikundi 302 vimepatiwa fursa ya kufanya matengenezo ya zaidi ya kilomita 1,500 za barabara katika maeneo mbalimbali nchini.

"Baada ya kuona mafanikio yaliyopatikana katika awamu ya kwanza, mwaka wa fedha 2026/27 tutaongeza wigo wa utekelezaji katika mikoa 25 ya Tanzania Bara, wilaya 70 na halmashauri 104," amesema Eng.Missa.

Ameeleza kuwa katika awamu hiyo, TARURA inalenga kuboresha zaidi ya kilomita 7,000 za barabara huku zaidi ya vikundi 1,400 vya wananchi vikitarajiwa kunufaika kupitia ajira zitakazotokana na shughuli hizo.

Kwa mujibu wa Eng. Missa, mpango huo una malengo mawili makuu ambayo ni kuhakikisha barabara zinakuwa katika hali nzuri na kupitika muda wote, pamoja na kuwapatia wananchi wanaoishi jirani na barabara hizo fursa za ajira.

Amefafanua kuwa shughuli zinazofanywa na vikundi hivyo ni pamoja na kuondoa nyasi pembezoni mwa barabara, kusafisha mifereji, makaravati na madaraja, pamoja na kuondoa vikwazo vinavyoweza kusababisha uharibifu wa barabara hasa wakati wa mvua.

"Matengenezo haya yanasaidia kuongeza uimara wa barabara kwa sababu changamoto ndogo zinazoweza kusababisha uharibifu mkubwa zinaondolewa mapema," amesema.

Aidha, amesema TARURA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imeanzisha mfumo unaowezesha vikundi vilivyosajiliwa kupata mikataba ya matengenezo ya barabara kwa urahisi zaidi kupitia taratibu za serikali.

Katika awamu ya kwanza, mpango huo unatekelezwa katika wilaya za Lushoto, Korogwe na Pangani mkoani Tanga; Rufiji na Mkuranga mkoani Pwani; Mvomero na Kilombero mkoani Morogoro; pamoja na Kongwa mkoani Dodoma.

Eng. Missa amesema mikataba inayotolewa kwa vikundi hivyo ni ya mwaka mmoja, huku shughuli za matengenezo zikifanyika kwa takribani siku 100 kwa mwaka ili kuwawezesha wanavikundi kuendelea na shughuli nyingine za kiuchumi.

Ameongeza kuwa vikundi hivyo pia vinapatiwa mafunzo ya ujasiriamali ili viweze kuendesha shughuli nyingine za kujiongezea kipato na kuwa endelevu hata nje ya kazi za matengenezo ya barabara.

Amesema kupitia Mpango wa CBRM, TARURA imetekeleza maelekezo ya Serikali ya kutenga asilimia 30 ya fedha za matengenezo ya barabara kwa ajili ya vikundi vya wananchi, hatua inayolenga kuboresha miundombinu, kuongeza ajira na kuinua uchumi wa jamii.

Post a Comment

Previous Post Next Post