Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mkoa wa Dar es Salaam umeendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi na matengenezo ya barabara, ikiwemo mradi wa DMDP II na upanuzi wa Bonde la Msimbazi, kwa lengo la kuboresha miundombinu na kurahisisha usafiri kwa wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Nyamagarura Masatu Ndango amesema mkoa huo unasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 5,057.7.
Amesema kati ya mtandao huo, asilimia 12.6 ni barabara za lami, asilimia 33.3 ni barabara za changarawe na asilimia 54 ni barabara za udongo.
Mbali na matengenezo ya kawaida ya mtandao huo, Eng. Ndango amesema TARURA inaendelea kutekeleza Mradi wa DMDP II, unaohusisha ujenzi na uboreshaji wa kilomita 191 za barabara katika halmashauri zote za Mkoa wa Dar es Salaam.
Ameeleza kuwa barabara hizo zinajengwa kwa kiwango cha lami na zitakuwa na mifereji ya maji ya mvua, taa za barabarani pamoja na njia za waenda kwa miguu, hatua inayolenga kuboresha usalama na kuongeza ufanisi wa usafiri mijini.
Aidha, amesema TARURA inashiriki katika utekelezaji wa mradi mkubwa wa upanuzi wa Bonde la Msimbazi, unaojumuisha ujenzi wa daraja lenye urefu wa mita 390, ujenzi wa kingo za Mto Msimbazi pamoja na kazi za kusafisha mto huo ili kupunguza athari za mafuriko.
Kwa mujibu wa Eng. Ndango, TARURA pia inaendelea na matengenezo ya kawaida ya barabara, matengenezo ya sehemu korofi, matengenezo maalumu, pamoja na ukarabati wa vivuko na madaraja madogo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Amesema utekelezaji wa miradi hiyo unalenga kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote wa mwaka, kuboresha huduma za usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi katika Jiji la Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, uongozi wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam umemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara, pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali wanaosimamia utekelezaji wa miradi hiyo.
