Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, amesema Tanzania na Misri zimeingia katika hatua mpya ya kuimarisha ushirikiano wa biashara, uwekezaji na miundombinu, akieleza kuwa ushirikiano huo unalenga kuongeza ustawi wa mataifa yote mawilikupitia viwanda, usafirishaji na biashara.
Ametoa kauli hiyo leo Julai 18, 2026 wakati akifungua rasmi Kongamano la Biashara Tanzania–Misri 2026 lililofanyika Hyatt Regency Dar es Salaam – The Kilimanjaro.
Prof. Mbarawa amesema kongamano hilo limefanyika sambamba na ziara ya kihistoria ya Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi nchini Tanzania kwa mwaliko wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku likiwa na kaulimbiu "Kutoka Mto Nile hadi Bahari ya Hindi: Ushirikiano wa Viwanda kwa Ustawi wa Pamoja."
Amesema ushirikiano wa nchi hizo umejengwa katika misingi ya urafiki wa viongozi waasisi Mwalimu Julius Nyerere na Gamal Abdel Nasser.
Ameutaja Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115, uliojengwa kwa ushirikiano wa kampuni za Arab Contractors na Elsewedy Electric kwa thamani ya dola bilioni 2.9 za Marekani, kuwa mfano wa mafanikio ya ushirikiano huo.
Aidha, amesema Elsewedy inaendelea kuzalisha mita za kisasa za umeme katika kiwanda chake cha Kigamboni kwa matumizi ya Tanzania na ukanda wa Afrika Mashariki.
Prof. Mbarawa ameendelea kwa kusema kuwa, biashara kati ya Tanzania na Misri ilifikia dola milioni 88.5 mwaka 2024, huku mauzo ya Tanzania kwenda Misri yakiongezeka kutoka dola milioni 4.8 hadi dola milioni 35.7 ndani ya mwaka mmoja.
Pia amesema Misri ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa nchini ikiwa na miradi 44 yenye thamani ya dola bilioni 1.4 na iliyozalisha zaidi ya ajira 4,000.
Vilevile ameeleza kuwa, Serikali mbili zinaendeleza mpango wa kituo cha kisasa cha usafirishaji kitakachounganisha Bandari ya Dar es Salaam na bandari za Sokhna na Safaga nchini Misri.
Kando na hayo, ametangaza kuwa timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Uchukuzi itakwenda Misri mwezi Julai kukamilisha Rasimu ya Mkataba wa Makubaliano (MoU) wa mradi huo.
Prof. Mbarawa amesema Tanzania inaendelea kuboresha Bandari ya Dar es Salaam, Reli ya Kisasa (SGR), barabara na madaraja ili kuongeza ufanisi wa usafirishaji.
