Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua meli nne mpya za mizigo zenye uwezo wa kubeba tani 2,000 kila moja katika hafla ya kitaifa itakayofanyika Julai 20, 2026 mkoani Kigoma, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na kuimarisha biashara katika ukanda wa Ziwa Tanganyika.
Akizungumza na waandishi wa habari, *Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mnyaa Mbarawa* leo Jumapili Julai 19, 2026 , amesema meli hizo zimetengenezwa na kampuni ya Gold Voyage Logistics Limited kutoka China na zitatoa mchango mkubwa katika kusafirisha mizigo kati ya Tanzania na nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Burundi na Zambia kupitia Ziwa Tanganyika.
Amesema uzinduzi huo unaenda sambamba na mkakati wa Serikali wa kuifanya Kigoma kuwa lango kuu la biashara kuelekea masoko ya Afrika ya Kati kwa kuimarisha usafiri fungamanishi unaojumuisha reli, bandari na usafiri wa majini kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Prof. Mbarawa amesema ongezeko la biashara katika ukanda huo linaonekana kupitia takwimu za Bandari za Ziwa Tanganyika zilizohudumia tani 815,285 za shehena katika mwaka wa fedha 2025/26, ikilinganishwa na tani 397,897 mwaka 2024/25, hali inayoonesha mahitaji makubwa ya miundombinu ya kisasa ya usafirishaji.
Ameeleza kuwa Serikali pia imejipanga kuboresha Bandari ya Kigoma kwa kujenga gati la kisasa la abiria na mizigo ili kuhudumia meli mpya pamoja na zilizopo, hatua itakayoongeza uwezo wa bandari hiyo kuhudumia biashara za ndani na za kimataifa.
Prof. Mbarawa amewaalika wananchi wa Kigoma na Watanzania kwa ujumla kushiriki hafla hiyo muhimu, akieleza kuwa miradi hiyo itaongeza fursa za biashara, uwekezaji na ukuaji wa uchumi wa Taifa huku ikiimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha usafirishaji katika ukanda wa Maziwa Makuu.
