Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, tarehe 18 Juni 2026 Mkoani Mara ameshiriki katika hafla ya kufunga mafunzo ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) yaliyofanyika mkoani humo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Dkt. Nyansaho amewapongeza washiriki wote kwa kujitokeza kwa wingi na kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo yaliyolenga kuwajengea uwezo wanawake katika nyanja mbalimbali za uongozi, siasa na maendeleo ya jamii.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa wanawake kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi, kudumisha mshikamano wa wananchi na kuimarisha misingi ya Chama Cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Dkt. Nyansaho ameeleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu muhimu ya mkakati wa kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kisiasa na kijamii, jambo ambalo linachangia kuimarisha maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Amesema wanawake wana nafasi kubwa katika kujenga jamii yenye ustawi, amani na maendeleo endelevu, hivyo ni muhimu kuendelea kuwapa fursa za kujifunza na kujiendeleza.
Kwa upande wake, uongozi wa UWT Mkoa wa Mara umeeleza kuwa mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa washiriki, kwani yamewapa maarifa na ujuzi unaohitajika katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi ndani ya chama na katika jamii.
Ziara hiyo ni sehemu ya ratiba ya viongozi wa chama ya kuendelea kuimarisha mawasiliano na wanachama, kusikiliza maoni yao pamoja na kutambua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali nchini, kwa lengo la kuendelea kuboresha huduma na kuharakisha maendeleo ya wananchi.
