UZUSHI WA KIONGOZI WA UPINZANI KUHUSU MATUMIZI YA MIKOPO YA MAENDELEO WAKATALIWA BUNGENI


Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, amesema madai yaliyotolewa na mmoja wa viongozi wa upinzani kwamba Serikali inakopa fedha lakini mikopo hiyo haionekani katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni uzushi usio na msingi na wenye lengo la kuwapotosha Watanzania.

Akichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027, Ulega amesema hakuna mkopo ambao Serikali imeuchukua na kushindwa kuutumia katika kutekeleza miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa wananchi.

Amesema ushahidi wa matumizi ya mikopo hiyo unaonekana wazi katika sekta ya ujenzi na uchukuzi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya barabara na viwanja vya ndege nchini.

Mhe. Ulega amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa anazoendelea kufanya katika kuharakisha maendeleo ya miundombinu nchini, akieleza kuwa maboresho yaliyofanyika katika viwanja vya ndege vya Tabora, Shinyanga na Sumbawanga pamoja na miradi inayoendelea katika viwanja vya ndege vya Kigoma na Tanga yamewezekana kutokana na mikopo nafuu inayopatikana kupitia wadau wa maendeleo.

Ameongeza kuwa Serikali pia inaendelea na mpango wa kujenga uwanja wa ndege wa kisasa wa Manyara, huku akisisitiza kuwa miradi hiyo yote imewezeshwa na mikopo ya maendeleo inayopatikana kwa masharti nafuu.

“Jambo la kusema tunakopa lakini hakuna jambo tunalolifanya ni uzushi, ni jambo lisilo na maana na lenye lengo la kuchonganisha Serikali na Watanzania,” alisema Ulega.

Amesema huenda kiongozi huyo wa upinzani hapendi kuona wananchi wa maeneo hayo wakinufaika kwa kutumia huduma bora za usafiri wa anga kupitia Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na viwanja vya ndege vilivyoboreshwa.

Aidha, amesema mikopo hiyo imewezesha ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato ambao utakuwa kitovu muhimu cha usafiri wa anga nchini na wenye uwezo wa kuhudumia ndege za aina mbalimbali.

Kwa upande wa miundombinu ya barabara, Ulega amesema mikopo hiyo imechangia ujenzi wa barabara ya njia sita kutoka Chamwino Ikulu hadi Dodoma Mjini pamoja na maendeleo ya mji wa kisasa wa Serikali katika Jiji la Dodoma.

Waziri huyo pia amesema Mkoa wa Kigoma umefunguka zaidi kiuchumi kutokana na utekelezaji wa miradi ya barabara ikiwemo Malagarasi–Uvinza na Kasulu–Manyovu, ambayo imewezekana kupitia mikopo ya maendeleo.

Amesema wananchi wanapaswa kupuuza taarifa za upotoshaji kuhusu mikopo ya Serikali kwa kuwa matokeo yake yanaonekana katika miradi mbalimbali inayotekelezwa nchini.

Ulega ameongeza kwa kusema kuwa, kupitia mikopo hiyo pamoja na maono ya Rais Samia, changamoto za mawasiliano katika baadhi ya maeneo ya kusini mwa Tanzania zinaendelea kupatiwa ufumbuzi kupitia ujenzi wa madaraja na barabara za kisasa.

Amelitaja Daraja la Somanga pamoja na madaraja mengine 81 yaliyojengwa nchini kuwa sehemu ya mafanikio yaliyopatikana kutokana na mikopo ya maendeleo.

Amesisitiza kuwa Serikali imefanya kazi kubwa katika kuboresha miundombinu ya nchi na inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuhakikisha sekta ya ujenzi na uchukuzi inachochea ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post