SERIKALI KUHAMASISHA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA ZA KISASA KATIKA SEKTA YA USAFIRI NA USAFIRISHAJI


Serikali imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya matairi ya Super Single katika sekta ya usafiri na usafirishaji nchini kwa lengo la kuongeza tija, kupunguza gharama za uendeshaji na kuimarisha ushindani wa huduma za usafirishaji katika soko la kikanda na kimataifa.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano jijini Dodoma na Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, wakati akizungumza mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, katika hafla ya uzinduzi wa Kituo cha Huduma za Magari na Mafunzo cha Kampuni ya Superdoll.

Prof. Mbarawa amesema Serikali inaendelea kupitia na kuboresha kanuni pamoja na taratibu mbalimbali ili kuweka mazingira wezeshi yatakayoruhusu matumizi ya teknolojia mpya zinazokubalika kimataifa, ikiwemo matumizi ya matairi ya Super Single ambayo yamekuwa yakitumika kwa mafanikio katika nchi mbalimbali za ukanda wa SADC.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha sekta ya usafiri nchini inaendana na mabadiliko ya teknolojia duniani na kuwawezesha wasafirishaji wa Tanzania kushindana kwa ufanisi zaidi katika masoko ya kikanda.

“Nchi nyingi za ukanda wa SADC zikiwemo Zambia, DRC na Zimbabwe tayari zinatumia teknolojia hii kwa mafanikio makubwa, hivyo kuna umuhimu wa kuendelea kuruhusu na kuhamasisha matumizi yake nchini ili kuongeza ushindani wa sekta yetu ya usafirishaji,” alisema Prof. Mbarawa.

Waziri huyo ameeleza kuwa matumizi ya matairi ya Super Single yana manufaa mbalimbali ikiwemo kupunguza matumizi ya mafuta kutokana na uzito mdogo na msuguano mdogo barabarani, kuongeza uwezo wa kubeba mizigo kwa ufanisi zaidi, kuimarisha uthabiti na usalama wa vyombo vya usafiri pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji na matengenezo.

Ameongeza kuwa, faida hizo zina mchango mkubwa katika kuongeza tija, kupunguza gharama za biashara na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha usafiri na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini.

Prof. Mbarawa yameendelea kwa kusema kuwa, umuhimu wa matumizi ya teknolojia hiyo unaongezeka kutokana na nafasi ya kimkakati ya Bandari ya Dar es Salaam katika kuhudumia biashara za nchi jirani.

Pia amebainisha kuwa hadi kufikia mwezi Machi 2026, zaidi ya tani milioni 10 za mizigo iliyohudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam zilielekezwa katika masoko ya nchi jirani hususan Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na mataifa mengine ya ukanda huo.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, ili wasafirishaji wa Tanzania waweze kushindana kwa usawa na wenzao wa nchi hizo, ni muhimu kuendelea kuruhusu matumizi ya teknolojia zinazosaidia kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi wa shughuli za usafirishaji.

Akizungumzia uwekezaji wa Kampuni ya Superdoll, Prof. Mbarawa amesema kituo hicho kipya cha huduma za magari na mafunzo kitakuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya usafiri kwa kuongeza ujuzi wa madereva na wataalamu wa usafirishaji, kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa na kuchangia kuimarisha usalama barabarani.

Amesema uwekezaji huo unaonesha mchango mkubwa wa sekta binafsi katika kuendeleza uchumi wa Taifa kupitia uwekezaji katika teknolojia, ubunifu na maendeleo ya rasilimali watu.

Hafla hiyo ya uzinduzi imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, mabalozi, viongozi wa sekta binafsi, viongozi wa dini pamoja na wadau wa sekta ya usafiri na usafirishaji kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post