REA YAZINDUA USAMBAZAJI WA MAJIKO BANIFU SONGWE, WANANCHI KUNUNUA KWA SH 12,200 TU


Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imezindua rasmi mradi mkubwa wa usambazaji wa majiko banifu mkoani Songwe. Mradi huo una thamani ya shilingi milioni 463.8, unalenga kuwasaidia wananchi kupata nishati safi na salama ya kupikia kwa bei nafuu.

Uzinduzi huo umefanyika leo tarehe 10 Juni, 2026 katika wilaya ya Mbozi, ukiongozwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Mhe. Hamad Mbega. Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano kati ya REA na kampuni ya ECOMAMA ICS Technology.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mhe. Hamad Mbega, amewataka wananchi, hasa akina mama, kuchangamkia fursa hiyo adhimu.

Hata hivyo, Mhe. Mbega ametoa rai kwa viongozi wa REA kuongeza idadi ya majiko hayo kutokana na idadi kubwa ya watu, alibainisha kuwa, katika mkoa mzima wa Songwe wenye wakazi takriban milioni 1.3, nusu yao wanaishi wilayani Mbozi na wengi wao wana mwamko mkubwa wa kutumia nishati safi.

Naye Meneja wa Miradi ya Nishati Safi mkoa wa Songwe, Bwana Vencha Maganga amesema mkoa wa Songwe umepata mgao wa majiko 6,488 ambapo kiasi cha shilingi milioni 463,892 zimetengwa kwa ajili ya zoezi hilo la usambazaji wa majiko hayo kwa njia ya ruzuku ambapo kila wilaya itapata mgao wa majiko 1,622 yenye thamani ya shilingi milioni 115,973.

“Ugawaji huu ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuondoa matumizi ya nishati zisizo safi na salama nchini pamoja na kulinda mazingira.” 

“Natoa wito kwa Wananchi wote, hususan wakina Mama kuchangamkia fursa hii ya majiko banifu ambayo kabla ya Serikali kutoa ruzuku; walipaswa kuyanunua kwa shilingi 71,500 lakini sasa Seikali imelipa shilingi 57,200 (Sawa na asilimia 80). Amekaririwa Bwana Maganga.

Bwana Maganga amezitaja wilaya zitakazonufaika na mgao huo kuwa wilaya ya Mbozi; Momba; Songwe na Ileje.

Mkurugenzi wa Kampuni ya ECOMAMA, Bi. Sabitina Makweta, amewahakikishia wananchi kuwa majiko hayo ni salama na yamethibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Aidha, Bi. Makweta alitaja sifa za majiko hayo kuwa ni ubanaji wa matumizi; yanatumia kuni kidogo na mkaa mchache na pia ni rafiki kwa mazingira.

“Yanaruhusu hewa safi ya oksijeni kupita kwa urahisi; yana uwezo wa kutumia kuni mbadala na mkaa mbadala pia.” Amesema Bi. Sabitina.

Post a Comment

Previous Post Next Post