Maofisa Uhusiano na Mawasiliano Serikalini wametakiwa kutengeneza simulizi zenye mvuto na tafsiri sahihi zitakazowasaidia wananchi kuelewa fursa mbalimbali zinazotekelezwa na Serikali kupitia miradi ya maendeleo nchini.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, wakati akiwasilisha mada kuhusu “Miundombinu kama Mhimili wa Ajira, Biashara, Huduma na Ushindani wa Taifa”katika Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Maofisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO) unaoendelea jijini Mwanza.
Bw. Msigwa amesema maofisa mawasiliano wanapaswa kutumia ubunifu na maarifa yao kueleza kwa wananchi mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia uwekezaji wa Serikali katika sekta ya miundombinu.
“Sekta hii ni muhimu na ina mchango mkubwa katika maendeleo ya taifa. Mna jukumu la kujenga uhusiano mzuri kati ya Serikali na wananchi ili waweze kufahamu kazi kubwa inayofanyika,” amesema.
Ameeleza kuwa miundombinu ni eneo mtambuka na kichocheo muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kuwa ndiyo msingi wa ajira, huduma, uwekezaji na fursa za kiuchumi zitakazoiwezesha Tanzania kufikia maendeleo endelevu.
Amesema kukamilika kwa miradi mikubwa ya miundombinu ikiwemo barabara na reli ya kisasa ya SGR kumeongeza ufanisi katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, biashara na usafirishaji.
“Ni wajibu wenu kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu miundombinu iliyotekelezwa na manufaa yake kwa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla,” amesema.
Aidha, amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unatarajiwa kuanza Julai 2026, huku miundombinu ikiwa miongoni mwa vichocheo vitano wezeshi vya utekelezaji wa Dira hiyo inayolenga kufikisha Tanzania kuwa Taifa Imara lenye uchumi jumuishi,shindani na linalojitegemea.
