Madereva kutoka Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wamekumbushwa umuhimu wa kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali na kulinda maisha ya watumiaji wa barabara.
Akitoa mafunzo maalum kuhusu usalama barabarani, Mkuu wa Kitengo cha Kikanda cha Umahili cha Usalama Barabarani kutoka Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Bw. Godlisten Msumanje, amesema dereva ana jukumu kubwa la kuhakikisha usalama wake pamoja na wa watumiaji wengine wa barabara.
Ameeleza kuwa uzingatiaji wa sheria za usalama barabarani ni njia muhimu ya kupunguza ajali ambazo zimekuwa zikisababisha vifo, majeruhi na hasara kubwa kwa familia na taifa kwa ujumla.
"Dereva anapokuwa barabarani anatakiwa kutambua kuwa ana wajibu wa kujilinda yeye mwenyewe na kuwalinda watumiaji wengine wa barabara. Tukizingatia wajibu huu, tutaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani," amesema Bw. Msumanje.
Aidha, amebainisha kuwa ajali za barabarani huathiri maendeleo ya jamii na uchumi wa taifa kutokana na kupoteza nguvu kazi muhimu pamoja na kuongeza gharama za matibabu na huduma nyingine za kijamii.
Kuhusu wajibu wa wananchi wawapo barabarani, mtaalamu huyo amewashauri wananchi umuhimu wa kutumia vivuko vilivyowekwa na kuhakikisha usalama wao kabla ya kuvuka barabara ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
Akizungumza kwa niaba ya kampuni ya UPIMAC iliyoratibu mafunzo hayo, Mratibu wa mradi, Mhandisi Daniel Msyani amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea madereva uwezo wa kutumia barabara kwa usalama na kuzingatia taratibu zote muhimu za usafiri.
"Mafunzo haya yamewakumbusha madereva wajibu wao wa kufuata sheria za usalama barabarani, kufanya ukaguzi wa magari kabla ya safari na kuchukua tahadhari zinazostahili ili kuzuia ajali zisizo za lazima", amesema Mhandisi Msyani.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Bw. Nestory Mushi na Bw. Paul Jeremiah kutoka TARURA, wamesema mafunzo hayo yamewapa maarifa mapya na kuwakumbusha hatua muhimu za kuzuia ajali pamoja na namna bora ya kutunza magari wanayotumia kutekeleza majukumu yao ya kazi.
Mafunzo hayo ya usalama barabarani yamehitimishwa jana mkoani Morogoro yakihusisha wataalamu mbalimbali kutoka TARURA na TANROADS wakiwemo wahandisi, maafisa usafirishaji na madereva.
