DKT. SHEKALAGHE AWASILISHA MKAKATI WA MIAKA MITATU WA RAIS SAMIA WA KUTOKOMEZA VIFO VYA UZAZI BARANI AFRIKA


Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, ameeleza mkakati wa miaka mitatu utakaoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika nafasi yake ya Bingwa wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, unaolenga kusaidia nchi za Afrika kupunguza na hatimaye kutokomeza vifo vya akina mama wajawazito vinavyoweza kuzuilika.

Dkt. Shekalaghe amesema hayo tarehe 13 Juni, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa Kikao cha Kamati ya Kitaalam (TWG 5) ya Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ahmad Mohammed Makuwani, mafanikio ambayo Tanzania imeyapata katika kuboresha afya ya uzazi, mama na mtoto ndiyo msingi unaoiwezesha nchi kushiriki kikamilifu katika juhudi za kikanda za kuboresha afya ya uzazi barani Afrika.

Dkt. Makuwani amesema kuwa tangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aanze kuongoza nchi, Serikali imeendelea kuwekeza katika afua za afya ya uzazi, mama na mtoto kwa kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa katika Mpango Mkakati wa RMNCAH One Plan III (2021/22–2025/26). Amesema mafanikio hayo yameifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazotajwa kama mfano wa kuigwa katika utekelezaji wa afua zinazolenga kupunguza vifo vya uzazi vinavyoweza kuzuilika.

Akifafanua mkakati huo, Dkt. Shekalaghe amesema Tanzania imeandaa andiko la dhana litakalotumika kama mwongozo wa kushirikisha mataifa mengine ya Afrika kujifunza kutokana na mafanikio ambayo Tanzania imeyapata licha ya kuwa na rasilimali chache.

"Baada ya kufanya tathmini ya mazingira ya kila nchi, tutaandaa viashiria muhimu vya kufuatilia maendeleo pamoja na afua mahsusi zitakazotekelezwa. Mfumo wa ufuatiliaji na tathmini utawekwa ili kuhakikisha hatua zinazochukuliwa zinaleta matokeo yaliyokusudiwa," alieleza Dkt. Shekalaghe.

Amesema lengo kuu la mpango huo ni kuhakikisha kuwa ifikapo mwisho wa kipindi cha miaka mitatu cha ubingwa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchi wanachama wa Umoja wa Afrika zitakuwa zimepiga hatua kubwa katika kuboresha afya ya uzazi na kupunguza vifo vya akina mama na watoto vinavyoweza kuzuilika.

"Tunaamini lengo hili linawezekana kufikiwa ikiwa nchi zitaendelea kushirikiana, kujifunza kutoka kwa uzoefu wa wenzao na kuwekeza katika afua zenye tija kwa afya ya mama na mtoto," amesema Dkt. Shekalaghe.

Post a Comment

Previous Post Next Post