ULEGA: DINI ZIUNGANISHE WATANZANIA , ZISIWAGAWE


Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amewataka Watanzania kuendelea kutumia dini kama mojawapo ya nguzo imara za kutunza amani na umoja wa taifa.

Waziri Ulega ameyasema hayo leo wakati wa uzinduzi wa Kanisa la Waadventista wa Sabato (SDA) la Musati, Musoma mkoani Mara ambapo alisema tofauti ya Tanzania na mataifa mengine ni kwamba wakati wengine wanagombanishwa na kutengana, hali ni tofauti hapa nchini.

“Angalia mfano wangu mimi. Naitwa Abdallah na dini yangu ni Muislamu. Kuna viongozi wengine wengi tu Wakristo ambao wangeweza kualikwa na kusingekuwa na shida. Lakini nimealikwa mimi Muislamu na ninyi mmenipokea kama mwenzenu,” alisema Ulega huku akishangiliwa na waumini wa Kanisa hilo.

Tukio la uzinduzi wa kanisa linalotajwa kuwa miongoni mwa yenye kuvutia zaidi nchini, lilihudhuriwa pia na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho na Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju.

Mbunge huyo wa Jimbo la Mkuranga mkoani Pwani alisema hata mafunzo ya dini karibu zote yanazungumzia kuhusu masuala yanayofanana ikiwemo umuhimu wa kupatana, kupendana na kumcha Mungu.

Akizungumza katika tukio hilo, Nyansaho alisema ujenzi wa Kanisa hilo hili umegharimu zaidi ya shilingi milioni 500 na zaidi ya kuwa nyumba ya ibada, kutakuwa pia na huduma nyingine za kijamii zitakatolewa kupitia jambo hilo.

Taasisi ya Nyansaho Foundation ni miongoni mwa taasisi na watu binafsi waliojitolea kwa dhati kuhakikisha ujenzi wa kanisa hilo unakamilika kwa wakati.

Post a Comment

Previous Post Next Post