TARURA ILEJE YAPEWA SIKU 14 KUKAMILISHA UJENZI WA DARAJA NA KURUDISHA MAWASILIANO


Serikali imetoa siku 14 kwa wakala wa barabara za Vijijini na Mjini (Tarura) wilayani Ileje mkoani Songwe kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa daraja la mto Luswiswi ili kuruhusu wanafunzi kuendelea na masomo

Iman Mtafya mkazi wa kijiji hicho amesema kwa sasa wanafunzi wameshindwa kupita katika daraja hilo, huku wengine wakitimkia shule nyingine, akiomba serikali kuwajengea hata la dharula ili kuruhusu mawasiliano.

“Tunaomba hata tupate daraja la muda kwa ajili ya wanafunzi, tusaidieni watoto waende shule, wengine wamehamia shule za jirani na mawasiliano yamekatika eneo hili, hiki ndicho kilio chetu” amesema Mtafya ambaye ni Katibu wa CCM Kata ya Rubanda.

Kwa upande wake Chabhola Mbali amesema Jimbo la Ileje limekuwa na bahati kuwa na mbunge ambaye amekuwa na mchango mkubwa kwa wananchi kwa kuwasikiliza na kuwatatulia kero zao.

“Wewe Kasekenya (Mbunge na Naibu Waziri) umekuwa nuru sana kwa wananchi wa Ileje, ujio wako kwenye jimbo mara kwa mara inatupa nguvu kutatuliwa matatizo, tufikishie salamu zetu Rais Samia Suluhu Hassan” amesema Mbali.

Naye Anangisye Kasebele amesema wanaishukuru serikali kwa kufika kijijini hapo kushuhudia changamoto zao, akieleza kuwa wanajivunia kuwa na Mbunge ambaye amekuwa na wananchi muda wote.

“Tunatoa shukrani kwa serikali namna inavyofika kwa wananchi kusikiliza na kutatua kero zetu, tunazo changamoto ya miundombinu ya madaraja kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha” amesema Kasebele.

Akizungumza na wananchi hao, Naibu Waziri Kasekenya amewataka Wakala wa barabara za Mjini na Vijijini (Tarura) wilayani humo kuhakikisha ndani ya siku 14 daraja hilo linatengenezwa ili kuruhusu wanafunzi kuendelea na masomo.

Hata hivyo ametumia nafasi hiyo kuwapa pole wananchi wa jimbo hilo kwa changamoto za barabara na daraja hilo, akieleza kuwa kutokana na tatizo hilo, mawasiliano yamekatika hivyo lazima juhudi za makusudi zifanyike.

“Tumekubaliana hiyo kazi ianze mara moja, Meneja wa Tarura yupo hapa, tumemkabidhi mkandarasi aanze kazi haraka, tunategemea isizidi wiki mbili iwe imekamilika ili shughuli ziweze kuendelea” amesema Kasekenya.

Mhandisi huyo na Mbunge wa Ileje ameishukuru serikali kwa kukubali ombi lake la kujenga daraja hilo akieleza kuwa anaamini kazi itafanyika na kukamilika kwa wakati, akieleza kuwa Rais ametoa kibali hivyo wananchi waendelee kuiamini serikali.

“Niishukuru serikali kwa ujumla kuanzia Rais, Tamisemi na Tarura kwa kuruhusu shughuli hii, tunataka watu wavuke kwa amani, watoto waendelee na masomo, hatutaki kupoteza maisha ya mtoto hata mmoja, mkandarasi siku 14 kazi imalizike” amesema Naibu huyo.

Kwa upande wake Meneja wa Tarura wilayani humo, Mhandisi Lugano Mwambingu amesema wanaamini ndani ya siku 14 kazi itakuwa imeisha na kuruhusu wanafunzi kuendelea na masomo na mawasiliano kurejea.

“Hii ni kazi ya dharula, bado hatujafanya tathimini kujua gharama ya mradi, lakini tutasimamia vyema kuhakikisha ndani ya siku 14 mkandarasi anamaliza kazi hii ili wanafunzi waendelee na shule ambayo inadaiwa kufungwa” amesema Meneja huyo.

Post a Comment

Previous Post Next Post