Serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia ya vinasaba nchini ili kuboresha huduma za afya, kuimarisha utoaji wa haki na kuchochea maendeleo ya kisayansi kwa manufaa ya taifa.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, alipomwakilisha Waziri wa Afya katika ufunguzi wa mkutano wa kisayansi wa teknolojia ya vinasaba uliofanyika jijini Dodoma, ukiwakutanisha wataalamu takribani 400 kutoka sekta mbalimbali.
Dkt. Samizi amesema teknolojia ya vinasaba ni nguzo muhimu katika utoaji wa huduma za kitabibu zenye ubora unaokubalika kitaifa na kimataifa, akieleza kuwa imekuwa na mchango mkubwa katika huduma za upandikizaji wa viungo kama figo na uroto wa mifupa, pamoja na utambuzi wa magonjwa na tiba za kisasa ikiwemo tiba jeni na utengenezaji wa chanjo.
Aidha, amesema teknolojia hiyo imeendelea kusaidia sekta ya haki jinai kwa kuwezesha upatikanaji wa ushahidi wa kisayansi katika uchunguzi wa makosa mbalimbali, hali inayochangia kuimarisha utawala bora na utoaji haki kwa wahusika.
Ameongeza kuwa Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika kuimarisha miundombinu, vifaa na rasilimali watu katika Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili kuhakikisha teknolojia hiyo inatumika kwa ufanisi.
Amebainisha kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa jengo la Ofisi na Maabara ya vinasaba vya binadamu lenye thamani ya shilingi bilioni 16.73, pamoja na ununuzi wa mitambo ya kisasa mitano ya uchunguzi wa vinasaba yenye thamani ya shilingi bilioni 3.5.
Dkt. Samizi amesema licha ya mafanikio hayo, bado kuna changamoto ikiwemo matumizi madogo ya teknolojia hiyo katika uchunguzi wa magonjwa ya kurithi na adimu, pamoja na matumizi hafifu ya tiba binafsishi na tiba jeni.
Ametoa wito kwa wataalamu kutumia mkutano huo kujadili kwa kina namna ya kuimarisha matumizi ya teknolojia ya vinasaba nchini, sambamba na kuibua mapendekezo yatakayosaidia Serikali kuboresha sekta hiyo kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.
Pia amesisitiza umuhimu wa wataalamu kuzingatia Sheria ya Udhibiti wa Vinasaba vya Binadamu, akionya dhidi ya vitendo vya kuchukua sampuli za vinasaba na kuzisafirisha nje ya nchi bila kufuata taratibu, hali inayoweza kuhatarisha usalama wa taarifa za watanzania.
