Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) umewatoa hofu Watanzania kuhusu upatikanaji wa mafuta nchini na kusisitiza kwamba yapo ya kutosha, na PBPA itaendelea kuhakikisha yanapatikana wakati wote.
Hayo yamesemwa na Meneja wa Sheria wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Bi. Lilian Rwegimbura leo Aprili 22, 2026 alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa na Clouds TV, kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, wakati wa Maonesho ya Wiki ya Nishati.
Alisema PBPA inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi mkubwa ili kuhakikisha nchi inakuwa na akiba ya mafuta ya kutosha, hata katika nyakati za changamoto za soko la kimataifa.
“PBPA tunafanya kazi kwa maslahi mapana ya Taifa. Uchumi wa nchi unategemea kwa kiasi kikubwa mafuta, hivyo sisi ni mhimili muhimu katika kuhakikisha shughuli za kiuchumi zinaendelea bila kukwama,” alisisitiza.
Akifafanua namna mfumo wa uagizaji mafuta kwa pamoja (BPS) unavyofanya kazi, Bi. Rwegimbura alisema PBPA hukusanya mahitaji ya mafuta kutoka kwa kampuni za mafuta (OMCs) na kuyaunganisha kabla ya kutangaza zabuni za kimataifa zilizo wazi na zenye ushindani.
“Zabuni hizi ni za ushindani na uwazi mkubwa, jambo linalotuwezesha kupata bei nzuri zaidi. Faida ya kuagiza kwa pamoja ni kupunguza gharama kupitia ununuzi kwa wingi (economies of scale),” alieleza.
Aidha, alibainisha kuwa PBPA imekuwa ikishirikiana kwa karibu na wafanyabiashara wa mafuta pamoja na taasisi za kifedha nchini ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kukua na kuwa imara.
