Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Ndugu Wazo Michael Mwang’onda, leo tarehe 16 Aprili 2026
ameweka Jiwe la Msingi katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Hondogo–Shija yenye urefu wa kilomita 4.16 kwa kiwango cha lami iliyopo katika wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza kabla ya uwekaji wa jiwe la msingi, Kiongozi huyo ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuendelea kutenga na kutoa fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya barabara, hatua inayochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa wilaya ya Ubungo na maeneo jirani.
Aidha, amesisitiza kwa mkandarasi kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo inatekelezwa kwa kuzingatia viwango vya ubora na kukamilika kwa wakati kama ilivyoainishwa kwenye mkataba, ili wananchi waweze kunufaika na huduma bora za usafiri na usafirishaji.
Sambamba na hilo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ametoa maelekezo mahsusi kwa mamlaka husika kuhakikisha wananchi wote walioathirika na mradi huo wanalipwa fidia zao ndani ya siku tano, ili kuwezesha utekelezaji wa mradi kuendelea bila vikwazo na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wananchi.
Mradi wa ujenzi wa barabara ya Hondogo–Shija (km 4.16) ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha miundombinu ya barabara mijini, kurahisisha usafiri na usafirishaji pamoja na kuchochea ukuaji wa shughuli za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa wilaya ya Ubungo na maeneo jirani.
