Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Ndugu Wazo Michael Mwang'onda, amekagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa barabara ya Mwakalinga yenye urefu wa kilomita 1.07 kwa kiwango cha zege iliyopo kata ya Chang’ombe wilayani Temeke mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi, Ndugu Mwang’onda amesema kuwa ameridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo na kuwataka wadau wote wanaohusika na ujenzi wa barabara hiyo kuhakikisha wanazingatia maelekezo aliyoyatoa ili mradi ukamilike kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
“Nimepokea taarifa kuwa ujenzi unaendelea vizuri. Nawapongeza sana wote mnaoshiriki katika utekelezaji wa mradi huu, lakini ni muhimu mkazingatia maelekezo yote niliyoyatoa ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa ubora unaotakiwa,” amesema Ndugu Mwang’onda.
Aidha, amemtaka Mkuu wa Wilaya, Mhe. Sixtus Mapunda, kusimamia ipasavyo utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Pia Kiongozi huyo ametoa maelekezo kwa TARURA kuhakikisha wanaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo, ikiwemo kuhakikisha mkandarasi anatekeleza kazi kwa kuzingatia viwango vya kitaalam pamoja na kukamilisha kazi zote za mifereji ya maji ya mvua ili kuondoa changamoto za maji katika eneo hilo.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Meneja wa TARURA wilaya ya Temeke Mhandisi Paul Mhere amesema kuwa mradi wa ujenzi wa barabara ya Mwakalinga ulianza tarehe 15 Januari 2026 na unatarajiwa kukamilika tarehe 11 Oktoba 2026 hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 65.
