Walimbwende 20 wanaoshiriki kinyang'anyiro cha kumsaka mnyange wa Tanzania ( Miss Tanzania) atakae wakilisha nchi katika mashindano ya ulimbwende duniani, yanayotarajiwa kufanyika nchini Vietnam kati ya Agosti na Septemba, 2026 wameahidi kuipeperusha SGR duniani kupitia mashindano hayo.
Walimbwende hao wametoa kauli hiyo Machi 13, 2026 waliposafiri na SGR kati ya Dar Es Salaam Dodoma kwa kutumia SGR, kwa lengo la kujifunza na kuongeza upeo.
Mkurugenzi wa kitaifa wa Shindano hilo Mustafa Hassanali, akizungumza mara baada ya kuwasili Dodoma, pamoja na mambo mengine amesema, walimbwende hao wameamua kutumia usafiri wa SGR kwakuwa wamelenga kupitia Miss World, kuiambia dunia kuwa Tanzania haina uzuri wa asili pekee , bali pia miundombinu ya kisasa na salama.
"Miss World ni jukwaa la kimataifa la kuibrand nchi husika, mashindano haya yana washiriki kutoka zaidi ya nchi 100 na huangaliwa na mamilioni ya watu duniani. Kufuatia hilo nchi zinazoshiriki hutumia fursa hii kuonyesha, mambo kadhaa kama utamaduni vivutio vya utalii,maendeleo ya kiuchumi na miundombinu" amemalizia Hassanali.
Katika hatua nyingine, baadhi ya walimbwende wanaoshiriki mashindano hayo wameeleza kufurahishwa kwao na usafiri wa SGR na kuahidi kuinadi nchini Vietnam ambako mashindano ya dunia yatafanyika kati ya Agosti na Septemba, 2026.
Silya Mussa mshiriki wa Miss World Tanzania ameipongeza serikali kwa ujenzi wa SGR ambayo imechochea kukua kwa sekta mbalimbali ikiwemo utalii na kama kijana ameahaidi kuinadi reli ya SGR katika Mashindano nchini Vietnam.
Kwa upande wake,Christina Mbaga, amesema endapo atafanikiwa kutwaa taji la Miss World Tanzania ameahidi kuinadi SGR kama ilivyo kwa vivutio vingine ikiwemo mbuga za wanyama, mito na madini.
Huduma za SGR zimekuwa chachu kubwa katika kuchagiza uukuaji wa kisekta nchini hivyo ni jukumu la Watanzania kuitangaza Sekta hii.
