Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Tume ya TEHAMA (ICTC) imeratibu mafunzo ya TEHAMA kwa vitendo wasichana 25 wa shule za awali jijini Dodoma, tarehe 16 Aprili, 2026.
Mafunzo hayo kuhusu nadharia mbalimbali za sayansi, ikiwemo mzunguko wa umeme yamefanyika kwa lengo la kuwajengea watoto hali ya udadisi katika umri mdogo, na kuwasaidia kupenda kujifunza masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati na kisha kujikita kwenye bunifu za sekta ya TEHAMA wanapokuwa wakubwa.
Jitihada hizi zinafanyika kuelekea maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Wasichana na TEHAMA, yatakayofanyika tarehe 23 Aprili, 2026 jijini Dodoma, ikiwa ni mpango mkakati wa Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) kuwahamasisha wasichana kupenda kusoma masomo ya STEM na kujikita kwenye tasnia ya TEHAMA ili kupunguza pengo lililopo kati ya wanawake na wanaume kwenye sekta hiyo
