Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, akiambatana na Mbunge wa Jimbo la Kibamba, Mhe. Angelah Kairuki, leo Aprili 12, 2026, ametembelea Kituo cha kulea watoto waliokuwa wanaishi na kufanya kazi mitaani cha Child in the Sun kilichopo Mbezi Makabe, mkoani Dar es Salaam.
Ziara hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto Anayeishi na Kufanya Kazi Mtaani, yenye kaulimbiu isemayo “Malezi na Ulinzi wa Mtoto ni Jukumu Letu Sote.”
Akiwa katika kituo hicho, Dkt. Gwajima ametembelea na kujionea utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo karakana ya ufundi, madarasa ya kujifunzia, uwanja wa michezo pamoja na miradi ya ufugaji inayolenga kuwawezesha watoto hao kujitegemea.
Katika hatua nyingine, Dkt. Gwajima amekabidhi zawadi mbalimbali kwa Mkurugenzi wa kituo hicho kwa ajili ya kusaidia watoto waliopo hapo, ikiwa ni ishara ya kuunga mkono juhudi za malezi, ulinzi na ustawi wa watoto hao.
