Ujumbe kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tarehe 6 Machi, 2026 umetembelea Makao Makuu ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) yaliyopo Mtumba jijini Dodoma kwa lengo la kujifunza mifumo inayotumika katika kulinda, kudhibiti na kusimamia hifadhi za barabara.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Kiongozi wa Ujumbe huo, Bi. Fatma Mohamed Ally, amesema lengo la ujio wao ni kuangalia mifumo ya TARURA ambayo wanaitumia hususan katika mipaka, usimamizi, udhibiti na kuangalia maeneo ambayk yanahitajika katika miundombinu ya barabara na yana umuhimu kijamii, kiuchumi na kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla.
“Tumekuja kuona na kujifunza mifumo inayotumika katika mipaka, usimamizi,udhibiti na maeneo yanayohitaji miundombinu ya barabara”.
Bi. Fatma amesema ziara hiyo imekuwa yenye mafanikio makubwa kwani mifumo waliyoikusudia kujifunza wameikuta ikitumika TARURA, huku akieleza kuwa kwa kiasi kikubwa inafanana na ile wanayotarajia kuianzisha Zanzibar.
“Naamini kwamba tutafikia mahali tutaenda sambamba na maelekezo ya Marais wetu wawili ambao wamekuwa wakiyatoa mara kwa mara kuhusu matumizi ya mifumo ya kidigitali katika shughuli za serikali”. Amesisitiza
Katika kikao na Menejimenti ya TARURA, ujumbe huo ulipata fursa ya kupitishwa katika maeneo mawili muhimu ya kiutendaji ambayo ni Mpango Endelevu wa Usimamizi wa Barabara pamoja na Mfumo wa Usimamizi wa Barabara za Wilaya (District Roads Management System – DROMAS).
Awali, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Edward Amboka, aliueleza ujumbe huo kuwa jukumu kuu la Wakala huo ni kusimamia ujenzi, ukarabati na matengenezo ya mtandao wa barabara za vijijini na mijini nchini.
Amesema mtandao huo una jumla ya kilomita 144,149.18 ambazo zilitangazwa rasmi kupitia Gazeti la Serikali Na. 314 la tarehe 13 Juni, 2025.
