TISEZA YAHAMASISHA FURSA ZA UWEKEZAJI BANDARI LA KAREMA



Ujumbe kutoka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) ukiendelea na ziara ya kuhamasisha uwekezaji mkoani Katavi, leo umetembelea eneo lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji lenye ukubwa wa ekari 179 lililopo karibu na Bandari la Karema, Wilayani Tanganyika mkoani humo.

Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kutambua na kuainisha fursa za uwekezaji zinazopatikana katika eneo hilo, hususan kutokana na ukaribu wake na bandari hiyo ya kimkakati ambayo ni lango muhimu la uchumi wa nchi, ikipokea na kusafirisha mizigo kuelekea nchi jirani za Burundi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Akizungumza na vyombo vya habari, Balozi Aziz Mlima amesema, “Bandari la Karema ni la kimkakati kwa kuwa ni mlango wa nchi za SADC kupitia Zambia. Jambo hili linasababisha eneo la ekari 179 lililotengwa na TISEZA kunufaika kwa kiasi kikubwa sana na soko la nchi za SADC.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TNCC Mkoa wa Katavi Bw. Zefrine Machesha aliyeambatana na ujumbe huo alitoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa hizo akisema, “Vijana, ajira ziko huku zinatusubiri sisi. Toka ulipo, tafuta fursa zilizopo ndani ya mkoa wako, zifanyie kazi na ujiajiri. TNCC tutakuongoza kwa kushirikiana na TISEZA.”

Naye Afisa Biashara wa Mkoa wa Katavi, Bw. Nhonge Thomas, amesema mkoa umejiandaa kupokea wawekezaji kwa kuchukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuandaa ofisi ya mkoa ya kuhudumia wawekezaji kwa kushirikiana kwa karibu na TISEZA, kuanzisha madawati ya uwekezaji katika halmashauri zote tano, pamoja na kila halmashauri kutenga ekari 500 kwa ajili ya miradi ya uwekezaji.

TISEZA inawakaribisha Watanzania wote kuwekeza mkoani Katavi, hususan katika eneo la Karema, ili kunufaika na fursa za kimkakati zilizopo na kuchangia maendeleo ya mkoa na Taifa kwa ujumla.

Post a Comment

Previous Post Next Post