Serikali imetoa msimamo ikisema Tanzania inayo mifumo ya kulinda haki za binadamu, ambayo ina vigezo vya kimataifa.
Msimamo huo ulitolewa leo na Balozi wa kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Dk. Alli Possi, alipofanya mkutano wake na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao.
Balozi Possi ambaye anahudhuria kikao cha 61 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC), kinachofanyika Geneva, Uswisi, alisema mifumo ya haki za binadamu iliyopo leo ni tofauti na mwaka 1961 nchi ilipopata uhuru.
Akifafanua zaidi uwepo wa mifumo hiyo, Balozi Possi alisema Katiba ya Uhuru ya Mwaka 1961 haikuwa na kipengele cha haki za binadamu, ulipofika mwaka 1988 Tanzania ilikiweka.
Kwa mujibu wa Balozi Possi, tangu hapo Tanzania imekuwa ikipiga hatua katika kulinda haki za binadamu kwa watu kuzidai hadi mahakamani na kuwepo Tume ikiwemo ya Utawala Bora.
"Naweza kusema ndiyo, tunayo mifumo ya kulinda haki za binadamu. Kwa mfano, Katiba yetu ya Uhuru ya mwaka 1961 haikuwa na vipengele vya haki za binadamu. Mwaka 1988 tuliviingiza. Tangu wakati huo wananchi wanazidai hadi mahakamani," alifafanua Balozi Possi.
Katika kuonyesha Tanzania inazidi kuimarisha mifumo hiyo, Balozi Dk. Possi alisema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan aliunda Tume ya Haki Jinai, ambayo ni sehemu ya kuboresha zaidi mifumo hiyo.
"Ndiyo maana Mheshimiwa Rais aliunda Tume ya Haki Jinai. Hii yote ni kufanya maboresho. Maboresho ni process. Hata hao walioemdelea zaidi hawajafika mwisho huwa wanafanya maboresho.
"Leo hapa kwetu hali ni tofauti. Uhuru upo, tunazungumza kwa uwazi, maboresho yanaendelea na hiiyo ni process," alisisitiza Balozi Dk. Possi.
TANZANIA INAJITATHIMIN
Kuhusu madai ya kuundwa Tume ya Uchunguzi ya Oktoba 29, kutoka nje, Balozi Possi alisema Tanzania haijafikia vigezo hivyo, kwani ina mifumo imara ya kijitathimini katika masuala ya haki za binadamu.
Alifafanua ,nchi inayoweza kuundiwa Tume ya nje ni ile ambayo haina mifumo madhubuti ya kujitathimini ikiwemo mahakama na au kama ilikaidi maelekezo ya Jumuiya ya kimataifa ikiwemo UNHRC.
Balozi Possi alisema hatua ya Tanzania kuunda Tume ya Uchunguzi ya Matukio ya Okgoba 29, ni uthibitisho kwamba haijakaidi masuala ya haki za binadamu na inaweza kujitathimini.
Alifichua kuwa jopo la Wajumbe wa Tume likiongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Chande, limejaa watu wenye weledi mkubwa na wanaoheshimika kimataifa.
Akitoa mfano wa Jaji Chande, alisema anaheshimika hadi Umoja wa Mataifa kwani ndiye anachunguza tuhuma za mauaji katika Mji wa el Fasher, Sudan ambako kuna mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
"Nitakuwa objective katika kujadili hili kuliko kuwa subjective. Ni sawa na glass, yupo mmoja anaweza kuona imejaa mwingine haikujaa. Muhimu tuipe nafasi Tume. Yenyewe ihoji watu wa kutosha kwa uwazi kabisa na hilo naamini linafanyika. Tusiwe kama wanasiasa, wakishinda kesi mahakamani wanasema mahakama ni huru wakishindwa wanasema haiko huru," alifafanua.
TASWIRA YA TANZANIA
Alisema wamekuwa wakiendelea na mijadala ya kidiplomasia kueleza hali halisi baada ya matukio ya Oktoba 29, kwa lengo la kuendeleza taswira nzuri ya nchi.
Balozi Possi alisema hadi hivi sasa Tanzania inaeleweka kimataifa, kwani imekuwa ikishiriki mijadala huru na wazi kuhusu mambo ya haki za binadamu na utekelezaji wa itifaki mbalimbali.
"Tunaendelea kufanya engagement na wenzetu. Tunazungumza kwa uwazi tu, " alifafanua.
Wiki hii, Kamshna Mkuu wa UNHRC, Volker Turk aliisifu Tanzania kwa mwenendo mzuri wa kulinda haki za binadamu kwa kuumda Tume huru ya Uchunguzi.
