NDEJEMBI: MIL. 704/- KUIMARISHA UMEME LINDI, MTWARA


Serikali imewekeza Sh.milioni 704 kufunga transfoma ya ziada katika kituo cha kupooza umeme cha Mahumbika mkoani Lindi ili kupunguza changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi ameyasema hayo alipokuwa akikagua maendeleo ya kituo hicho katika muendelezo wa ziara yake ya kukagua miradi ya umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Ndejembi amesema kufungwa kwa transfoma hiyo ni jitihada za muda mfupi za Serikali katika kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi wa mikoa hiyo.

“Pamoja na jitihada hizi za muda mfupi, bado kuna mradi mkubwa wa kusafirisha umeme kutoka Songea kupitia Tunduru hadi Masasi na hatimaye kufika Mahumbika, ambao utaongeza nguvu ya upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara,” amesema.

Amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya kuimarisha miundombinu ya umeme katika ukanda huo, ikiwemo mradi wa kusafirisha umeme kutoka Mkuranga kupitia Somanga, Kilwa hadi Lindi, ambao utaunganishwa na miundombinu ya kusambaza umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Aidha, Ndejembi ameipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kuhakikisha wakandarasi waliotekeleza ujenzi wa kituo hicho ni wazawa kutoka ndani ya taasisi hiyo.

Amesema pia Serikali ina mpango wa kuhakikisha kila wilaya inakuwa na kituo chake cha kupooza umeme (substation) ili kupunguza changamoto za kukatika kwa umeme zinazosababishwa na hitilafu katika maeneo mengine.

“Hatutaki tena hali ya umeme kukatika Mtama kwa sababu ya hitilafu iliyotokea Lindi Mjini au Nachingwea. Lengo ni kuhakikisha kila wilaya inapata substation yake, na haya ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa kuongeza transfoma katika kituo cha Mahumbika, Joseph Efrem, amesema kufungwa kwa transfoma mpya yenye uwezo wa 15 MVA kumeongeza uwezo wa kituo hicho kufikia takribani MVA 35.

Amesema hatua hiyo itaongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme na kusaidia kuimarisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara.

Post a Comment

Previous Post Next Post