MBUNGE PONDEZA ATOA SADAKA YA FUTARI KWA WAJANE 360 JIMBO LA CHUMBUNI


Waumini wa dini ya Kiislamu wametakiwa kutimiza nguzo ya nne ya Kiislamu kwa kufanya ibada kwa moyo mkunjufu ili kuweza kufikia lengo la funga.

Akizungumza katika ugawaji wa futari kwa akina mama waliofiwa na waume zao (wajane) katika hafla iliyofanyika skuli ya Dkt. Salmin Amour, Mbunge wa Jimbo la Chumbuni Mhe. Ussi Salum Pondeza amesema zoezi hilo la ugawaji futari ni miongoni mwa hatua ya kuwafariji na kuwasaidia wajane ili waweze kushiriki ibada swaum ya mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa utulivu.

Amesema katika zoezi hilo amefanikiwa kuwafikia wajane 360 kwa shehia zote zilizopo jimboni humo ikiwa ni sehemu ya kuendeleza mshikamano na kusaidia jamii katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Jimbo la Chumbuni Mhe. Makame Mohamed Sufian amesema, ataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha makundi maalum yanapatiwa msaada hususan kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan ambapo mahitaji huongezeka.

Nao wajane waliopatiwa msaada huo, Mariam Nassoro Mwinyi na Asia Seif Khamis wameishukuru ofisi ya mbunge na mwakilishi wa Jimbo la Chumbuni kwa kuwajali na kuwakumbuka huku wakisema msaada huo umewapa faraja na matumaini katika maisha yao ya kila siku.

Post a Comment

Previous Post Next Post