Katibu wa NEC, Itikadi,Uenezi na Mafunzo CCM Kenani Kihongosi akiwa wilaya ya Bukoba mjini ametembelea nakukagua mradi wa Soko la kisasa pamoja stand ya Mabasi Manispaa ya Bukoba.
Kenani amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya hiyo katika Manispaa ya Bukoba, mradi uliokuwa ukisubiriwa kwa zaidi ya muongo mmoja lakini kufanikishwa ndani ya kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo unaogharimu takribani Sh bilioni 18.9, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi alisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya kweli ya serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha ahadi kwa wananchi zinatekelezwa kwa vitendo.
Kihongosi alifafanua kuwa fedha zinazotumika kutekeleza mradi huo zimetokana na mkopo wa Benki ya Dunia, akibainisha kuwa si msaada wa bure bali ni fedha zinazopaswa kurejeshwa, hali inayodhihirisha uamuzi wa serikali kuwekeza kwa makusudi katika miradi ya maendeleo.
Alisema ubora wa ujenzi unaoendelea unaendana na thamani ya fedha iliyowekezwa, jambo linaloonesha matumizi sahihi ya rasilimali za umma na usimamizi mzuri wa mradi huo mkubwa.
Aidha, aliwapongeza wahandisi na mkandarasi wanaotekeleza mradi huo kwa kazi nzuri wanayoifanya, akieleza kuwa kiwango cha ujenzi kinatia matumaini na kuakisi weledi wa wataalamu wa ndani.
Katika hatua nyingine, aliwatambua vijana wanaoshiriki katika ujenzi huo kwa juhudi zao, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha wanalipwa stahiki zao kwa wakati ili kuongeza morali na ufanisi kazini.
Alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya biashara kwa wakazi wa Bukoba na kuchochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo kwa ujumla.
Pia alizitaka mamlaka za wilaya kuweka utaratibu wa haki kwa wafanyabiashara waliokuwepo awali ili wapewe kipaumbele cha kupata nafasi katika soko hilo mara litakapokamilika, hatua itakayosaidia kuepusha malalamiko yasiyo ya lazima.
Soko hilo litakuwa na jumla ya vizimba 1,848, maduka 234 (yakiwemo 132 ya chini na 102 ya juu), huduma mbalimbali za kijamii, ofisi nne, pamoja na maegesho ya magari madogo 47, magari makubwa 32 na mabucha 12.
