Katika kuendelea kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha uwekezaji wa ndani, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imetembelea kiwanda cha Organic Foods Katavi Limited kilichopo wilayani Mpanda, kinachozalisha maji yanayojulikana kwa jina la Baridi Kata Kiu.
Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Bw. Alhassan Radack, amesema uzalishaji wa maji ulianza mwezi Aprili 2025 na tayari kiwanda kimetoa ajira kwa Watanzania 110. Ameeleza kuwa wakati anaanza ujenzi wa kiwanda hakufahamu kuhusu TISEZA na vivutio vyake, ambavyo vingemsaidia kupunguza gharama za uwekezaji kwa kiasi kikubwa.
Bw. Radack ameongeza kuwa kwakukwa ana mpango wa kupanua mradi kwa kuanzisha uzalishaji wa vinywaji baridi(soda),ameahidi kujisajili TISEZA ili kunufaika na vivutio vya kikodi na visivyo vya kikodi. Miongoni mwa manufaa hayo ni huduma ya kituo cha mahali pamoja (_One Stop Facilitation Centre_)kwa ajili ya vibali mbalimbali, pamoja na msamaha wa ushuru wa forodha kwa asilimia 75 wakati wa kuingiza mitambo, malori na vifaa vya vingine vya uzalishaji.
Kwa upande wake, Meneja Uhamasishaji Uwekezaji wa TISEZA, Bw. Felix John, amempongeza Bw. Radack kwa uwekezaji wake na uamuzi wa kujisajili TISEZA. Aidha, amewahamasisha Watanzania wengine kuiga mfano wa Organic Foods Katavi Limited ili kuongeza kasi ya uwekezaji kwa maendeleo ya Katavi na Taifa kwa ujumla.
