WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba leo Februari 18, 2026 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Mwanga ambalo ujenzi wake utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 3.9.
Akizungumza baada ya kuweka jiwe hilo la msingi, Waziri Mkuu amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amewaagiza wasimamizi wa ujenzi wa hospitali hiyo kuhakikisha wanaendelea kufanya kazi kwa viwango na kukamilisha maeneo yote ambayo yamebaki ili wananchi waendelee kunufaika na huduma za afya.
Ujenzi wa hospitali ya wilaya utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma za afya kwa wananchi kwa kuwapatia huduma karibu na maeneo yao, hali itayosaidia kupunguza vifo hususani kwa mama na mtoto.
Majengo yaliyokwishakamilika na kuanza kutoa huduma katika hospitali hiyo ni pamoja na jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la mionzi, maabara na stoo ya dawa (pharmacy). Aidha, ujenzi wa jengo la wodi ya uzazi, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la kufulia pamoja na kuchomea taka unaendelea.
