AWESO AMUHAKIKISHIA WAZIRI MKUU MRADI WA MAJI ZIWA CHALA KUANZA HARAKA


Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amemuhakikishia Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) kuwa Wizara ya Maji haitakuwa kikwazo katika utekelezaji wa Mradi wa Maji kwa kutumia chanzo cha Ziwa Chala na ndani ya siku 14 watakuwa wamekamilisha mchakato wa kumpata mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo.

Ahadi hiyo imetolewa kufuatia agizo la Waziri Mkuu Dkt. Nchemba alilolitoa wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Marangu–Kitowo, Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro. 

Dkt. Nchemba amesisitiza kuwa ujenzi wa mradi huo unapaswa kuanza mara moja, akieleza kuwa ni suluhisho muhimu la changamoto ya upatikanaji wa maji inayokabili Wilaya nzima ya Rombo. Ameeleza kuwa Serikali imedhamiria kuona wananchi wanapata huduma bora na ya uhakika ya majisafi na salama.

Kwa mujibu wa Waziri Aweso, Wizara ya Maji imejipanga kuhakikisha mchakato wa kumpata mkandarasi unakamilika ndani ya muda uliopangwa ili kuruhusu ujenzi kuanza bila kuchelewa na kukamilika kwa wakati.

Aidha, Waziri Aweso ameelezea mafanikio ya miradi ya maji iliyotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, ikiwemo miradi ya Njoro, Mahorosha–Msaranga–Wona, Marangu Endument na Kinyasini Usaiwambushi, akibainisha kuwa miradi hiyo imeimarisha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wananchi wa maeneo husika.

Mradi wa Maji Ziwa Chala unatarajiwa kugharimu Sh. bilioni 8.66 na utanufaisha wananchi 34,104 katika vijiji 14 vya Wilaya ya Rombo, hatua itakayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.

Post a Comment

Previous Post Next Post