Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amesema atahakikisha pikipili 300 alizokabidhiwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Bashiru Ally kwa niaba ya Maafisa Ugani nchini, zinatunzwa na kutumika kutoa elimu na mafunzo kwa wakulima sio kwa shughuli za bodaboba.
Prof. Shemdoe hayo leo katika Viwanja vya Makumbusho ya Taifa Jijini Dar es Salaam, mara baada ya kupokea pikipiki 300 kwa niaba ya Maafisa Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Prof. Shemdoe amemshukuru Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Bashiru Ally pamoja na watendaji wa wizara yake, kwa kuona umuhimu wa kuwapatia Maafisa Ugani vitendea kazi vitakavyo wawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
“Nikuhakikishie tumepokea pikipiki hizi na tutahakikisha zinatunzwa na zinaenda kufanya kazi iliyokusudiwa, na hazitoonekana zikifanya shughuli za bodaboda,” Prof. Shemdoe amesisitiza.
Aidha, Prof. Shemdoe amemhakikishia Mhe. Dkt. Bashiru Ally kuwa, pikipiki hizo zitatumika pia katika zoezi la chanjo kwani Maafisa Ugani ni miongoni mwa maafisa wanaoshiriki kwenye kampeni ya chanjo nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt. Bashiru Ally amesema wizara yake inatambua changamoto zinazoikabili sekta ya mifugo nchini ikiwepo ya utoaji wa huduma za ugani, na katika mwendelezo wa kutatua changamoto hizo wizara yake kuanzia mwaka wa fedha 2023/24 hadi 2024/25 imeshanunua jumla ya pikipiki 2200 ambazo zimeshasambazwa kwa Maafisa Ugani nchini.
Sanjari na hilo, Dkt. Bashiru amesema kuwa Wizara yake imeshanunua vishikwambi 4500, vifaa vya chanjo ikiwemo ‘cool box’ 3270, ‘automatic syringe. 3370 na ‘Gun boots’ 2180 na kuwapatia Maafisa Ugani katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili waendelee kuimarisha huduma za ugani ikiwemo utekelezaji wa zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo.
Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea na jitihada zake za kuwawezesha kiutendaji watumishi wa umma walio katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, kwa kuwapatia vitendea kazi vitakavvowarahisishia kutoa huduma bora kwa wananchi.
