Leo Jumatatu Disemba 15, 2025 Mkoa wa Kagera umeandika historia baada ya Makamu wa Rais wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi kuweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Tawi la Kagera. Ikumbukwe mpaka sasa mkoa huu unaosifika kwa wasomi hauna Chuo Kikuu hivyo hii inakua fursa kwa Vijana na wananchi kupata Elimu ya juu ndani ya mkoa.
Afisa Tarafa Katerero Ndugu Bwanku M Bwanku ameshiriki kikamilifu kwenye tukio la uwekaji Jiwe la Msingi wa ujenzi Chuo hiko kwenye Kijiji cha Itahwa Kata ya Karabagaine Wilaya ya Bukoba.
Ujenzi wa Chuo hiki unagharimu Bilioni 14 na mpaka sasa mradi huu mkubwa wa kisasa na wa aina yake umefikia asilimia 78. Mwaka wa masomo 2026/27 masomo yanatarajiwa kuanza rasmi Chuoni hapo kikitarajiwa kuanza na Shahada (Degree) 3 za biashara, tehama na uhasibu.
Mradi huu wa ujenzi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam utabadilisha mkoa wa Kagera na kufungua fursa mbalimbali za vijana na wananchi wa Kagera na Tanzania kwa ujumla ikiwa ni dhamira ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kutawanya maendeleo kila mahali kwa wananchi.
Tukio hili lilihudhuriwa pia na Rais Mstaafu wa Awamu ya 4 ambaye ndiye Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, viongozi mbalimbali wa mkoa na wilaya na wananchi.
