TANZANIA YATEULIWA KUWANIA TUZO ZA UTALII DUNIANI 2025


Tanzania imechaguliwa kuwania Tuzo za Utalii Duniani za mwaka 2025, katika vipengele vinne vya juu zaidi duniani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Ofisi za Tuzo za Utalii Duniani  (WTA) kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, Tanzania imeteuliwa katika vipengele vifuatavyo:Eneo bora zaidi duniani kwa utalii 2025, fukwe bora za kanda Duniani 2025 kupitia Fumba Beach, Tanzania, eneo bora zaidi Duniani kwa utalii wa safari 2025, Bodi bora zaidi Duniani ya Utalii 2025 ambayo ni Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Uteuzi huo unaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa machache yanayowania heshima kubwa zaidi katika sekta ya kimataifa ya utalii na usafiri, jambo linaloonesha mafanikio makubwa ya jitihada za serikali katika kukuza sekta hiyo muhimu.

Kwa mujibu wa WTA, upigaji kura unafanyika kuanzia Oktoba 6 hadi 26, 2025, ambapo wataalamu wa usafiri, vyombo vya habari, na watumiaji wa huduma za utalii duniani kote watashiriki kumchagua mshindi. 

Uteuzi huo unaendelea kuthibitisha nafasi ya Tanzania kama moja ya vituo bora zaidi vya utalii barani Afrika na duniani, hususan kutokana na vivutio vyake vya kipekee kama Hifadhi ya Serengeti, Mlima Kilimanjaro, na fukwe za Zanzibar.

Pia, Mgombea atakayepata kura nyingi zaidi atatangazwa mshindi katika hafla ya kimataifa ya utoaji wa tuzo hizo mwaka 2026.

Post a Comment

Previous Post Next Post