Mgombea ubunge wa Jimbo la Mwanga kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ngwalu Maghembe, ameeleza kuwa wananchi wa jimbo hilo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto kubwa ya wanyamapori hususan tembo, ambao wamekuwa wakiharibu miundombinu na mazao ya wananchi, hali inayohatarisha maisha na maendeleo ya jamii.
Akihutubia mkutano wa kampeni uliohudhuriwa na Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, Maghembe alisema tatizo la tembo limekuwa kubwa katika kata nane za tambarare ambapo wanyama hao wamekuwa wakibomoa miundombinu ya maji, kuharibu mashamba na wakati mwingine kusababisha vifo vya binadamu.
> “Serikali tayari imeweka ofisi ya tawi pale kwa kona, lakini bado inakabiliwa na upungufu wa fedha, magari na askari. Tukipata msaada huu, wananchi watakuwa salama na hata tembo nao watalindwa na kurudishwa hifadhini,” alisema Maghembe.
Mbali na changamoto ya tembo, Maghembe aligusia pia umuhimu wa kuboresha barabara zinazohudumiwa na TANROADS katika Jimbo la Mwanga. Alitaja barabara ya kichwa cha ng’ombe yenye urefu wa kilomita 82 inayozunguka maeneo ya mlima hadi Kifaru, ambayo alisema ipo katika hali mbaya na imekuwa kikwazo kwa wananchi.
Aidha, alieleza kuwa barabara za Kifaru–Langata, Lembeni–Shirati na ile ya kuelekea Butiama, ambazo ujenzi wake umeshafikia asilimia 60, zinahitaji kukamilishwa ili kuchochea uchumi wa wananchi.
> “Moja ya kero kubwa ni miundombinu duni ya barabara. Kwa mfano, kuna basi moja tu asubuhi na jingine usiku, na hii ni kwa sababu ya ubovu wa barabara. Tukiboresha miundombinu hii, wananchi watanufaika kiuchumi na kijamii,” alisisitiza.
Maghembe pia alieleza matumaini yake kuwa serikali ya CCM itaendelea kushughulikia changamoto nyingine ikiwemo afya, elimu na stendi ya mabasi, ambazo tayari zimeanza kufanyiwa kazi.
Alimalizia kwa kumshukuru mgeni rasmi Dkt. Nchimbi kwa kuungana nao na kueleza kwamba anaamini changamoto hizo zitapata suluhisho kupitia serikali ya chama hicho.
