Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango Dkt. Fred Msemwa amesema Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2050 inakuja wakati sahihi zaidi kutokana na utayari mkubwa wa kupiga hatua kama Taifa kutokana na uwepo wa miundombinu bora ya kiuchumi inayowezesha shughuli za kiuchumi kufanyika vizuri kuliko wakati wowote.
Dkt. Fred amebainisha hayo leo Jumatatu Julai 14 wakati akihojiwa na Runinga ys Taifa Mjini Dodoma, ikiwa ni siku tatu kabla ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua rasmi Dira 2050 Mjini Dodoma kwenye Ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, akiwaalika wananchi wote kuhudhuria tukio hilo la Kihistoria ambalo hutokea mara moja kila baada ya miaka 25.
"Dira 2050 inakuja wakati ambapo Tanzania ina utayari mkubwa zaidi wa kupiga hatua kubwa kuliko wakati wowote katika historia ya nchi yetu, ikiwemo elimu kwa Watanzania, miundombinu ya sasa ya kiuchumi kama barabara, reli, usafiri wa anga, usafiri wa majini kwasasa pia ipo tayari zaidi kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika kirahisi zaidi kuliko wakati wowote na maarifa ya watanzania pia ni makubwa katika kutambua rasilimali zetu na kuzitumia."
"Kazi yetu sasa kama wananchi ni kuhakikisha kwamba tunatumia vyema vitu hivi ili kuharakisha maendeleo yetu kwasababu tunazo rasilimali zote zinazohitajika kupiga hatua na ndio maana ya Dira 2050 kuainisha vitu gani ni vya muhimu zaidi vitakavyotupeleka mbele kwa kasi zaidi." Ameongeza kusema Dkt. Msemwa.
Aidha akizungumzia upekee wa Dira 2050, Dkt. Msemwa amebainisha kuwa Dira hiyo ndiyo Dira shirikishi zaidi kuliko nyingine zote zilizopita, wananchi mmoja mmoja zaidi ya Milioni moja na laki mbili walifikiwa, semina, makongamano na mitandao ilitumika kupata maoni ya wananchi.
Akizungumzia kwa uchache miongoni mwa yaliyosemwa zaidi wakati wa ukusanyaji maoni Dkt. Msemwa ameeleza kuwa Watanzania wengi wametaka maboresho ya mifumo ya elimu nchini, wakitaka wahitimu wawe na uwezo wa kujitegemea, kufanya kazi, kujiajiri na kuwa na uwezo, ubunifu na maarifa yatakayowafanya wahitimu kuweza kushindana kwenye soko la ajira.
Aidha wananchi wengi pia walitaka maboresho kwenye huduma za afya pamoja na matumizi sahihi ya rasilimali za Taifa ili kuweza kuwanufaisha watanzania wote.
Katika uzinduzi wa Dira 2050 siku ya Alhamisi, wananchi na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wanaofikia zaidi ya 5, 000 wanatarajiwa kuhudhuria uzinduzi huo ikiwemo washirika wa maendeleo, Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa zilizopo nchini, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Vyama vya siasa pamoja na wakuu wa Taasisi za Umma na Binafsi zilizopo nchini.