BAADA YA JINA LAKE KUKATWA; ALEX MSAMA ATOA NENO


Siku moja tu baada ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuondoa jina lake miongoni mwa watia nia wa Jimbo la Ubunge Ukonga jijini Dar, aliyetia nia, Alex Msama ametoa neno zito.

Msama ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Msama Promotions & Dira Media ametoa neno kwa kuwataka watia nia wote waliokatwa majina yao nchini kote kutoa ushirikiano kwa wale ambao majina yao yanakwenda kupigiwa Kura za Maoni ngazi ya kata na hatimaye kumpata mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya CCM kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Huyu hapa Alex Msama: "Nilitia nia kuomba kuteuliwa na chama changu kugombea Ubunge Jimbo la Ukonga. Lakini isivyo bahati jina langu halikurudi.

"Siyo kwamba sifai. Nafaa ila jina langu halikurudi. Kwa wakati huu wamepatikana wengine ambao wamepewa nafasi na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya chama chetu ili kuendelea na mchakato.

"Sisi sote ni wana CCM. Kwa hiyo wote tuna sifa ila waliopitishwa wanafaa kwa sasa. Nawaomba watia nia wengine wote ambao pia majina yao hayakurudi, tuwape ushirikiano wale ambao majina yao yamerudi. Hiki ni kipindi cha kushikamana badala ya kusambaratika. 


"Kwa hiyo niwaombe wale wote waliotia nia kama mimi lakini majina yao hayakurudi, tushikamane kwa nia ya dhati ya kuendelea kukiweka chama chetu katika umoja ili kumsaidia Mwenyekiti wa CCM-Taifa. Mama yetu, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan."

Msama aliendelea kusema kuwa, katika kipindi hiki hategemei kuwepo kwa makundi kwa sababu ya majina yao kutorudi au kukatwa.

Akasema: "Kama watia nia wenzangu walimsikiliza vizuri Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Amos Makalla baada ya kumaliza kusoma majina yaliyorudi, alisema wote ambao majina yao hayakurudi tuwe watulivu bado chama kina mahitaji mengi. Kwa hiyo tutulie na kushikamana."

Aidha, Msama alisema kuwa, wazo la viongozi wa CCM kuamua kurekebisha taratibu ya kurudisha majina mengi badala ya matatu kama ilivyokuwa awali ni wazo la busara na la maana sana.

Alisema: "Awali ilikuwa majina yanayokwenda ngazi ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa ni mengi. Lakini yaliyotakiwa kurudi kwa ajili ya kupigiwa kura za maoni ni matatu tu. Mwenyekiti wetu akaona siyo mpango mzuri. Kwa sababu wengi wana sifa. Akaamua majina yote yaende ngazi ya juu na kurudi yarudi zaidi ya matatu kwa sababu wenye sifa ni wengi.

"Ndiyo maana baadhi ya majimbo yamerudi majina hadi kumi. Kusema kweli hili lilikuwa wazo la busara sana kwa chama chetu ambacho kinashika dola na kuwaongoza Watanzania. 

"Nampongeza sana mwenyekiti wetu wa taifa na wana CCM wezangu wa wilayani ambao waliunga mkono kwenye mkutano uliyoitishwa kwa njia ya mtandao," alisema Msama.

Aidha, Msama aliwataka Watanzania wote ambao wana sifa ya kupiga kura kwenye uchaguzi ujao (2025) na wamejiandikisha, kujitokeza kwa wingi siku ya tarehe 29, Oktoba kwa ajili ya kupiga kura huku akisisitiza kuwa, Tiki iende kwa Samia Suluhu Hassan. 

"Kwa sasa nchi yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo kwenye harakati za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2025. Wapo wananchi wamejiandikisha kupiga kura kwa sababu wana sifa. Nawaomba wajitokeze kwa wingi siku ya tarehe 29, Oktoba ili kumchagua rais, wabunge na madiwani. Lakini kama ni kutiki, tutiki kwa CCM," alimaliza kusema Msama.

Post a Comment

Previous Post Next Post