SERIKALI YATENGA BILIONI 32 KUIMARISHA CHUO CHA MICHEZO MALYA


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amesema Serikali imetenga Shilingi Bilioni 32 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya nyongeza katika Chuo cha Umahiri wa Michezo Malya, kwa lengo la kuimarisha chuo hicho na kukabiliana na uhaba wa wataalam wa michezo nchini.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Ngudu, wilayani Kwimba, mkoani Mwanza, Mhe. Majaliwa alieleza kuwa Serikali inaendelea kujikita katika kuhakikisha taifa linakuwa na wataalam wa kutosha na wenye ujuzi wa kufundisha michezo, ili kuinua sekta hiyo muhimu.

“Pamoja na jitihada zinazofanyika kwenye michezo, tumegundua bado tuna tatizo la wataalam. Kwa hiyo, Mheshimiwa Rais ametenga Bilioni 32 ambazo zitaletwa Kwimba, ziende Malya kujenga majengo ya chuo cha umahiri wa michezo,” amesema Mhe. Majaliwa. “Tunaposema chuo cha umahiri, tunamaanisha tupate viongozi wa kuongoza michezo Tanzania.”

Aidha, Waziri Mkuu ameongeza kuwa katika sekta ya elimu, Serikali inaendelea kujenga shule mpya ili kupunguza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu.

Post a Comment

Previous Post Next Post