Serikali tayari imefuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa nyumba zote zinazojengwa zikiwa chini ya thamani ya Sh Milioni 50 ili kuboresha maendeleo ya makazi kwa wananchi wake.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Deogratius Ndejembi kwenye ufunguzi wa Mkutano Mkuu na Kongamano la tano la Chama cha Wataalamu wa Miliki Kuu Tanzania (AREPTA), na Mkutano wa Mwaka wa Chama cha Wataalamu wa Miliki Bara la Afrika Kanda ya Afrika Mashariki jijini Arusha, Mei 15, 2025.
“Katika sera za mwanzo kutungwa baada ya nchi yetu kupata Uhuru ni Sera ya Nyumba, sasa kwa chochote kile kitakachoweza kutusaidia kuchochea kuwa na makazi bora, sisi kama Serikali tupo tayari kushirikiana nanyi. Tayari tumeshachukua hatua mbalimbali ikiwemo kuondoa VAT kwa nyumba zozote zinazojengwa chini ya unit ya Sh Milioni 50,” amesema Mhe. Ndejembi.
Amesema Serikali tayari imeanza kupitia upya sera na sheria mbalimbali ili kuhakikisha kuwa maendeleo katika sekta ya miliki yanaendana na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii ambapo tayari Rais Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan alishazindua Sera ya Taifa ya Ardhi ya Mwaka 1995 Toleo la Mwaka 2023 ambapo sera hiyo pamoja na masuala mengine inatambua mchango wa sekta miliki katika ukuaji wa uchumi wa Pato la Taifa.