MBUNGE MAVUNDE AWATAKA MACHINGA STENDI KUU NANENANE KUCHANGAMKIA FURSA ZA MIKOPO YA ASILIMIA KUMI


Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde ametoa rai kwa  Umoja wa wamachinga Stendi Kuu ya Mabasi nanenane(UWASIDO) kuchangamkia fursa za mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani inayotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Mh. Mavunde ameyasema hayo jana wakati wa mkutano wake na Wamachinga wa Stendi kuu nanenae Jijini Dodoma kusikiliza kero na changamoto zao sambamba na kutimiza ahadi yake ya kuwapatia sare wamachinga 600 wa eneo hilo la Stendi.

“Tunaishukuru serikali chini ya Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan kwa uendelezaji wa mradi huu mkubwa wa Stendi na hivyo kuwapa fursa ya kufanya biashara katika eneo hili.

Nafahamu changamoto kubwa kwa sasa mliyonayo ni upatikanaji wa mitaji ya kuwawezesha kukuza na kuendeleza biashara zenu.

Nitoe rai kwa uongozi kuona namna bora ya uanzishwaji wa SACCOS ya Wamachinga ili kuongeza wigo mpana wa upatikanaji wa fursa za kiuchumi ikiwemo mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Jiji inayolengwa kwa ajili ya wakina mama,Vijana na Watu wenye ulemavu.

Katika kuanzisha SACCOS hiyo nitawachangia Tsh 10,000,000 ya kianzio”Alisema Mavunde

Naye Diwani wa Kata ya Nzuguni Mh. Alloyce Luhega ameishukuru serikali kwa ujenzi wa mradi huo ambao umesaidia kuchochea maendeleo ya eneo pamoja na kutoa fursa kwa wananchi wengi kujiingizia mapato kupitia biashara mbalimbali zinazofanyika hapo.

 Naye Mwenyekiti wa UWASIDO Ndg.   Hadson Lesilwa ameipongeza serikali kwa mradi wa stendi ya mabasi ambao umetoa fursa kwa kundi kubwa la wananchi kujiajiri kupitia shughuli za biashara mbalimbali na kuiomba Halmashauri ya Jiji Dodoma kuwatengea eneo ili kuwa rasmi na kufanya biashara zao kwa uhakika.

Aidha Mweyekiti Lesilwa amemshukuru Mbunge Mavunde kwa kuwa nao bega kwa bega kwenye utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili na kwa kutimiza ahadi yake ya kuwapa sare machinga wote wa Stendi kuu Nane Nane

Post a Comment

Previous Post Next Post