MAENEO YALIYOTUMIWA NA WAPIGANIA UHURU KUWA VIVUTIO VYA UTALII


Wizara ya Maliasili na Utalii inatarajia kutangaza baadhi ya maeneo yaliyotumiwa na wapigania uhuru wa kusini mwa Afrika kuwa vivutio vya utalii wa kihistoria, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kukuza na kuendeleza sekta ya utalii nchini.

 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula ameyasema hayo bungeni leo alipokuwa akijibu swali la Mhe. Dkt. Rita Kabati, ambaye ametaka kufahamu iwapo kuna mpango wa kuyatambua na kuyaendeleza maeneo kama Kihesa Mgagao (Kilolo) ili yawe vivutio vya utalii.

Mhe. Kitandula akijibu swali hilo, amebainisha kuwa maeneo kama Kihesa Mgagao – Kilolo na Mazimbu – Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, Kampasi ya Mazimbu, tayari yamepata ridhaa kutoka kwa wamiliki wake ili yachukuliwe hatua stahiki na kutangazwa kuwa sehemu ya urithi wa taifa.

Aidha, ameongeza kuwa Wizara inaendelea na zoezi la kubaini maeneo yenye historia na umuhimu wa kihistoria ambayo yanaweza kuendelezwa kama vivutio vya utalii. Maeneo hayo yanajumuisha yale yanayomilikiwa na Halmashauri za Manispaa na Wilaya, Taasisi za Serikali na binafsi, pamoja na jamii na familia mbalimbali. Baada ya utambuzi huo, Serikali huanzisha majadiliano na wamiliki ili kuweka mikakati ya kuyaendeleza

"Tanzania, chini ya uongozi wa Awamu ya Kwanza wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ilijipambanua kuwa mstari wa mbele katika harakati za ukombozi wa nchi nyingi za Kusini mwa Afrika. Serikali ya wakati huo ilitoa maeneo maalum kwa wapigania uhuru kwa ajili ya kujenga makambi ya mafunzo ya kiitikadi na kijeshi, ambapo wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi walihusika katika kuwaandaa wapambanaji wa ukombozi wa mataifa yao,"amesema

Amesema hatua hiyo ya Serikali inalenga kuhifadhi historia, kuuenzi mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Afrika, pamoja na kuvutia watalii wa ndani na nje wanaopenda kujifunza historia ya bara hilo.

Post a Comment

Previous Post Next Post