MADAKTARI BINGWA ARUSHA WAJIPANGA KUWAFIKIA WANANCHI 7000


Katibu Tawala wa mkoa wa Arusha Bw. Missaile Musa amesema kuwa wamejipanga kuwahudumia wananchi wapatao 7000 kwenye kambi ya madaktari bingwa wa Rais Samia iliyoanza leo kwenye Halmashauri saba (7) za mkoa huo.

Bw. Missaile ameyasema hayo Mei 12, 2025 alipokuwa akipokea jopo la Madaktari Bingwa wa Rais Samia wapatao 50 watakaoweka kambi kwa muda wa siku sita (6) na kutoa huduma za kibingwa mkoani hapo.

"Mkoa tupo tayari kuwapokea na kuwapa ushirikiano wa kutosha muda wote wa kambi, Mganga Mkuu wa mkoa yupo, msisite kuwasiliana naye kwa lolote ili kambi yetu iweze kuleta tija tuliyokusudia," amesema Bw. Misaile.

Bw. Missaile amekiri wananchi katika maeneo yao kukabiliwa na changamoto za kiafya na wengine kushindwa kuzifikia huduma za Kibingwa kutokana na umbali, hivyo uwepo wa madaktari Bingwa wa Mama Samia itakuwa ni ukombozi kwao kwani huduma zitawafikia mahali walipo.

Kwa Upande wake Mratibu wa zoezi hilo kwa mkoa wa Arusha kutoka Wizara ya Afya Bi. Notgera Ngaponda, amesema mbali na kutoa huduma kwa wananchi mabaingwa hao pia watatumika katika kuwajengea uwezo wataalam wa Afya waliopo kwenye vituo.

"Kambi hizi sio tu, zinakwenda kutatua changamoto za kiafya bali pia kuwajengea uwezo wenzetu ngazi ya msingi sambamba na kuanzishwa kwa huduma ambazo zilishindwa kuanza kutokana na changamoto ya utaalam wa kibingwa," amesema Bi. Notgera.

Kwa upande wa Mganga Mkuu wa mkoa wa Arusha Dkt. Charles Mkombachepa amesema, wanamshuru Rais Samia kwa kuwakumbuka wananchi wa mkoa wa Arusha kwa mara nyingine tena ikiwa ni awamu ya tatu.

"Kila tulipoandaa kambi hizi tulipokea wananchi hata kutoka nje ya mipaka ya mikoa, hii inamaanisha kuwa, watu wana changoto za Afya lakini hawajui wanazifikia vipi huduma za kibingwa hivyo ujio wenu ni fursa kwetu wananchi kujitokeza kuangaliwa afya zetu," amesema Dkt. Mkombachepa.

Mkoa wa Arusha umepokea madakatari bingwa wa watoto, kinamama, upasuaji, usingizi na ganzi salama, kinywa na meno, koo, pua na masikio, magonjwa ya ndani na wauguzi wakunga mabingwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post