"Kwa heshima kubwa na unyenyekevu wa dhati nimesimama mbele yenu kwaniaba ya jumuiya ya Mawakili Zanzibar katika tukio hili muhimu la uzinduzi wa kampeni ya Kitaifa ya huduma ya msaada wa kisheria inayofanya kazi Tanzania nzims hususani nizungumze kwa visiwa vyetu vya Zanzibar.
Mhe. Mgeni rasmi leo hatuzindui tu kampeni bali tunathibitisha dhamira ya haki, usawa na ulinzi thabiti wa haki za binadamu kwasababu msaada wa kisheria sio anasa bali ni haki. Haki inayohakikisha kuwa kila mwananchi bila kujali hali yake ya kiuchumi na nafasi ya kijamii, ya kisiasa au ya kijiografia anapata haki na ulinzi wa mali zake kisheria.
Msaada wa kisheria ni daraja kati ya sheria zilizoandikwa na haki halisi. Bila msaada huu haki hubaki kuwa maneno tu kwenye makaratasi. Kampeni hii inalenga kuongeza uelewa, kupanua huduma na kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika kupata usaidizi wa kisheria, ushauri na uwakilishi.
Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na wizara ya Katiba, utumishi na utawala bora Zanzibar kwa pamoja na wadau wengine wa maendeleo imechukua hatua hii muhimu ili kuhakikikusha kila mwananchi anakuwa na sauti mbele ya sheria, anapata usaidizi wa kitaalamu anapokabiliwa na changamoto za kisheria na zaidi ya yote anaheshimiwa na watu wote kwa kulinda haki zake za msingi. Ushirikiano huu umejengwa juu ya maono ya pamoja, Zanzibar yenye haki kwa wote, heshima ya haki za binadamu na utawala wa sheria pamoja tutajenga programu endelevu za msaada wa kisheria mijini na vijijini.
Kampeni hii iwe wito wa kuchukua hatua kwa wanasheria na kwa taasisi na kwa kila mwananchi katika kushirikiana kujenga jamii yenye haki zaidi ambapo kila sauti inasikika na kila haki inalindwa
Tukiwa hapa leo tuitazame huduma hii kama chombo cha kuimairisha misingi ya haki, usawa na uwajibikaji katika jamii yetu tukikumbuka kuwa Taifa lenye amani ya kweli ni lile linalojenga mazingira ya haki kwa wote bila kujali itikadi za kisiasa, za kiuchumi, kijamii na za kiografia.Upo msemo mashuhuri pia wa Papa Paulo wa sita aliyesema kama unataka amani fanyeni haki.
Zanzibar kwakweli tuna uhitaji wa msaada hasa kwa wale watu ambao hawawezi kwenda mahakamani au kwenye vyombo vya kisheria kudai haki zao. Kazi ipo ya kujitahidi kufika huko ndani, chini kabisa, kuna watoto wananyanyasika, wanadhalilishwa, kuna watoto hawasomi wakiamka asubuhi wanaenda kuvunja mawe hawapati muda wa kwenda skuli ama madrasa na wanakuwa hawana elimu yoyote sio ya duniani wala ya akhera. Hili ni jukumu lote sote, tunapaswa kuifanya hii kampeni kwa vitendo kwelikweli."- Wakili Joseph Magazi, Rais Jumuiya ya Mawakili Zanzibar