Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ametekeleza kwa vitendo maagizo ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango ya ujenzi wa chuo cha wauguzi kitakacho jengwa pembeni ya hospitali ya Wilaya ya Rombo Mkoani Kilimanjaro.
Waziri Mhagama amesema hayo leo Januari 7, 2024 akiwa katika ziara ya siku mbili Mkoani Kilimanjaro kwa lengo la kukagua na kuzindua miradi ya sekta mbalimbali ikiwemo ya Sekta ya afya katika Wilaya ya Rombo pamoja na Wilaya ya Same ambapo leo amezindua wodi ya wazazi iliyopo katika Kituo cha Afya Mkuu - Rombo.
"Ndugu zangu Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan haijawahi kupoa, hasa kwenye Sekta ya Afya, tupo macho kupokea maelekezo na kuyatekeleza, sasa ujenzi wa chuo chetu cha wauguzi utaanza mwezi wa tatu ili kupunguza tatizo la watumishi ndani ya Wilaya, Mkoani na Tanzania kwa ujumla," amesema Waziri Mhagama
Waziri Mhagama amesema tayari Wizara ya Afya imetenga shilingi Bilioni Moja ili kuanza haraka iwezekanavyo ujenzi huo ambao utakua na uwezo wa kuchukua vijana zaidi ya mia sita na vijana wa bweni wasiopungua mia nne.
Aidha, Waziri Mhagama amesema ndani ya miaka Mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali yake imetoa shilingi Bilioni 82 katika Wilaya ya Rombo ili kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo miradi katika sekta ya afya ikiwemo ya ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya, zahanati pamoja na hospitali.
"Tunaposema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni wa viwango vya juu tunamaanisha kwa sababu miaka iliyopita Rombo haijawahi kupokea fedha nyingi kiasi hiki na hizo Bilioni 82 ni kati ya Bilioni 956 zilizoletwa katika mkoa huu wa Kilimanjaro, tunakila sababu ya kumshukuru Rais kwa kuamua kuibeba Tanzania ikiwemo Mkoa wa Kilimanjaro kwa kiwango tofauti," amesema Waziri Mhagama
Katika hatua nyingine Waziri Mhagama amewataka Watanzania kuzingatia ufanyaji wa mazoezi pamoja na ulaji wa vyakula kwa kupunguza mafuta, chumvi na sukari ili kuepuka kupata magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari na shinikizo la juu la damu (presure).
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu amemshukuru Rais Dkt. Samia kwa mapenzi makubwa ya wananchi wake wa mkoa huo, ambapo katika kipindi cha miaka mitatu mkoa huo umepokea shilingi Bilioni mia 656 za maendeleo.
"Katika hizo shilingi Bilioni 656 tumepokea Bilioni 117 kwa ajili ya maendeleo katika sekta ya afya na tunaendelea na ukarabati na ujenzi wa miundombinu pamoja na ununuzi wa vifaa, vifaa tiba na dawa ili wananchi waendele kupata huduma bora na salama za afya," amesema Mhe. Nurdin Babu