Jamii imekuwa haina uelewa mkubwa wa ugonjwa wa usonji (Autism) hali ambayo inazuia watoto wengi wenye hali hii kutopata msaada unaohitajika. Hivyo inachangia changamoto kubwa katika familia na jamii kwa ujumla, kwani watoto wenye usonji mara nyingi wanahitaji msaada maalum ili waweze kujiendeleza na kushiriki katika jamii.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na mshauri wa Rais katika masuala ya Afya, Prof. Lawrence M. Janabi, wakati akizungumza kuhusu hali ya usonji nchini Tanzania. Prof. Janabi amesema kuwa, ugonjwa huu hujitokeza mapema, mara nyingi kabla ya mtoto kufikisha miaka mitatu, na takwimu za kimataifa zinaonesha kuwa kati ya watoto mia moja, mmoja anapata ugonjwa huu.
“Usonji ni hali inayohusisha changamoto katika mawasiliano, uhusiano wa kijamii na tabia zinazojirudia. Hata hivyo, jamii nyingi nchini Tanzania bado hazijaelewa vya kutosha kuhusu dalili za ugonjwa huu, na hii inawaathiri watoto wengi katika kupata huduma muhimu,” amesema Prof. Janabi.
Prof. Janabi amefafanua dalili kuu za usonji ambazo ni pamoja na changamoto katika mawasiliano, ambapo watoto wenye ugonjwa huu wanapata ugumu kuelewa mifano, kejeli au mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja. Aidha, alieleza kuwa watoto hawa pia wanakutana na changamoto katika kuelewa na kujibu hisia za watu wengine, huku tabia zao zikiwa zinazorudiarudia na kuwa na upinzani wa mabadiliko katika ratiba au mazingira.
“Wazazi na walezi wanapaswa kutafuta msaada hospitalini kwani wataalamu wataweza kuwasaidia kuelewa na kushughulikia changamoto wanazokutana nazo. Ni muhimu kuwa na ufahamu wa kina kuhusu hali hii ili kuhakikisha watoto wanapata matibabu na huduma zinazostahili,” ameongezea Prof. Janabi.
Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa Decoder Health na Mtafiti wa Masuala ya Tiba ya Tabia (Applied Behavior Analysis) kutoka Marekani, Dkt. Annie Laswai, amesema
kuna programu ya mafunzo ya tabia kwa watoto wenye usonji ambayo itaanza hivi karibuni kwa kushirikiana na Hospitali ya Muhimbili. Programu hiyo itatolewa kupitia Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUCOHAS) na inalenga kuwapa wataalamu na wazazi ujuzi wa kufanya kazi na watoto wenye usonji ili kuboresha huduma zinazotolewa kwao.
Dkt. Laswai aliongeza kuwa programu hii itasaidia kuongeza ufanisi katika matibabu ya watoto na kutoa msaada kwa familia ambazo zinahitaji kuelewa na kushughulikia hali ya watoto wao wenye usonji.